Zaidi ya watu milioni 40 wafuatilia mikutano CCM

By Romana Mallya , Nipashe Jumapili
Published at 06:03 PM Oct 05 2025
Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo  CCM, Kenan Kihongosi
PICHA: CCM
Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM, Kenan Kihongosi

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimetoa tathmini ya mikutano yake ya kampeni iliyofanyika hadi sasa katika mikoa 21, kikisema zaidi ya watu milioni 14.62 wamejitokeza moja kwa moja na milioni 31.6, wamefuatilia kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo  CCM, Kenan Kihongosi, ameyasema hayo leo Oktoba 5, 2025, wakati akitoa tathmini ya mikutano ya kampeni kwa mgombea urais, Dk. Samia Suluhu Hassan na mwelekeo wao.
Kihongosi amesema mpaka sasa mgombea urais amefanya mikutano 77 katika mikoa hiyo 21, baada ya uzinduzi uliofanyika Agosti 28, 2025, katika Viwanja vya Tanganyika
Packers, Kawe, Dar es Salaam. 
 “Dk. Samia ameshafanya mikutano 77, katika mikoa 21, kwenye kanda za Kati, Magharibi, Pwani, Kusini, Nyanda za Juu Kusini, Pemba na Unguja (Zanzibar), vilevile Kanda ya Kaskazini. 
“Mikutano yote hiyo, kanda kwa kanda, mkoa hadi mkoa, mahudhurio yamekuwa makubwa. Hiyo ni kuonesha jinsi mgombea
wetu anavyokubalika, na wananchi kwa mamilioni, wameweka imani kubwa kwake.
“Imani ya wananchi kwa Dk. Samia Suluhu Hassan, siyo bahati wala mkumbo, bali ni imechagizwa na uongozi wenye mafanikio makubwa katika miaka minne aliyoshika usukani wa urais,”amesema.
Ametaja mafanikio hayo ni pamoja na  kutekeleza mradi wa Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere (INHPP), alioupokea ukiwa asilimia 37 hadi kufikisha asilimia 99.55. 
Amesema Samia amefanya vema kwenye miradi ya miundombinu, kuanzia Reli ya Standard Gauge (SGR), kutoka Dar es Salaam mpaka Makutupora (Km 722), kisha mapinduzi makubwa ya usafiri wa treni kati ya Dar es Salaam na Dodoma
“Ndani ya miaka minne ya uongozi wake, Dk Samia amejenga kilometa, ndege mpya sita za abiria na moja ya mizigo zimenunuliwa, hivyo kufanya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), kuwa na ndege 16,” amesema.
Amesema ametekeleza miradi 1,633 ya usambazaji wa maji imekamilika, miongoni mwa hiyo, miradi 1,335 ni ya vijijini peke yake.
Kihongosi amesema amekamilisha Daraja la Busisi (Daraja la Magufuli) pamoja na ujenzi wa chanzo cha maji cha Butimba, kinachowanufaisha wananchi 450,000 Mwanza. 
“Kufanikiwa kwa mradi wa maji ya Ziwa Victoria, unawahudumia wananchi 86,980 wa Tinde na Shelui.
“ Ujenzi wa vivuko sita Ziwa Victoria vimekamilika na kuanza kazi. Boti ya kuhudumia majeruhi wa ajali (Ambulance), Ziwa Victoria,” amesema.
Amesema chanjo ya mifugo imezinduliwa na Shilingi bilioni 62 imetolewa.  “Hayo na mengine yaliyofanyika, Dk.Samia bado ana fungu la neema kwa watu wa Kanda ya ziwa.