Zitto: Nipelekeni bungeni nikapiganie fidia zenu

By Halfani Chusi , Nipashe Jumapili
Published at 12:49 PM Sep 21 2025
Mgombea Ubunge Jimbo la Kigoma Mjini kupitia tiketi ya Chama Cha ACT Wazalenndo Zitto Kabwe
PICHA:MPIGAPICHA WETU
Mgombea Ubunge Jimbo la Kigoma Mjini kupitia tiketi ya Chama Cha ACT Wazalenndo Zitto Kabwe

Mgombea Ubunge Jimbo la Kigoma Mjini kupitia tiketi ya Chama Cha ACT Wazalenndo Zitto Kabwe, amesema akishinda ubunge ataenda kupigania wananchi ambao hawajalipwa fidia ya ardhi na serikali kwa kisingizio cha kujengwa kwa miradi ya maendeleo.

Zitto ameyasema hayo leo Septemba 20 akiwa Kamala kata ya Bangwe, jimbo la kigoma mjini katika mwendelezo wa kampeni zake za kusaka kura katika jimbo hilo akisisitiza kitendo kilichofanywa na serikali ni kinyume Cha katiba.

Aidha amesema atasiamamia suala la usalama kwa wavuvi na vyombo vyao Ili waweze kujikwamua kiuchumi kupitia biashara hiyo na kwamba wanapaswa kuifanya kazi hiyo kwa amani na usalama.

"Ninafahamu watu wa Bangwe wanahitaji Kituo Cha Afya, ninajua wapi kwa kupata fedha za ujenzi wa kituo nipeni kura zenu ili nikaifanye kazi hii" amesema Zitto huku akishangiliwa na wafuasi wa chama hicho.

Amesema yeye haendi bungeni kufanya uchawa ili apendelewe bali anakwenda kuwasemea wanajimbo wake na ikibidi atafoka kuhakikisha wanapata maendeleo. "Nimefanya hivyo Kigoma Kaskazini nilikuta hakuna barabara hata moja iliyojengwa kwa kiwango cha lami kwa muda mfupi  nimeacha km 100" amesema Zitto 

Aidha ameahidi akishinda ubunge ataanzisha mfuko na ataweka Sh billion moja kwaajili ya kuwakopesha wajasiliamari bila riba ili waachane na mikopo ya kausha damu inayowafanya waishi bila amani.

Kuhusu kufungwa ziwa amesema hakuna sababu ya kisayansi na kwamba akishinda ubunge halitafungwa tena kama ambavyo hawajalifinga mwaka huu. "Mkimpeleka Mbunge zwazwa bungeni hata ona hayo niliyoyaeleza, nipelekeni bungeni Ili nikawasemee tuweze kuivusha Kigoma" amesema Zitto huku akiwaomba wananchi hao kumpa kura za ndio