Mchungaji wa Kanisa la Mandate and Power Ministries International, Mtumishi wa Yesu Dk. Mandate Josephat, amesherehekea siku yake ya kuzaliwa kwa kugusa maisha ya watoto wenye uhitaji kwa kutoa misaada mbalimbali katika vituo vya watoto yatima jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo la utoaji misaada, Dkt. Josephat amesema kuwa anatambua changamoto za maisha kutokana na maisha ya umasikini aliyotokea, hivyo anaona ni wajibu wake kuwarudia wahitaji sasa baada ya kubarikiwa.
“Nimetoka katika familia ya kipato cha chini. Baada ya Mungu kunibariki, nimejiwekea utaratibu wa kusaidia wenye shida mbalimbali huu ndio mfumo wa maisha yangu. Tangu tuanze utumishi huu, tumesaidia zaidi ya vituo 90 vya watoto yatima hapa Dar es Salaam,” alisema Dk. Josephat.
Ameongeza kuwa mbali na kusaidia vituo vya yatima, pia huchangia ujenzi wa vituo vya ibada chini ya kanisa lake.Misaada iliyotolewa ilijumuisha magunia ya mchele, unga, tambi, sabuni pamoja na fedha taslimu kwa ajili ya mahitaji mbalimbali ya watoto hao.
Vituo vilivyonufaika na msaada huo ni pamoja na Al-Madina (Tandale), Afic Intensive Care and Rehabilitation Home, New Life Dar es Salaam, na Makao ya Watoto Kurasini kinachomilikiwa na Serikali.
Kwa upande wao, watoto waliopokea misaada hiyo walimshukuru Mchungaji huyo kwa moyo wake wa upendo na kumkumbuka katika siku yake ya furaha. Walisema msaada huo utawasaidia kwa mahitaji ya kila siku, ikiwemo nauli ya wanafunzi na matumizi mengine muhimu. Aidha, watoto hao waliwaomba watu binafsi na taasisi mbalimbali kuiga mfano wa Dk. Mandate Josephat kwa kuwasaidia watu wenye uhitaji katika jamii.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED