MACHIFU 200 wa mikoa tisa ya Kanda ya Kusini, wanatarajiwa kufanya matembezi maalumu mkoani Mbeya kwa lengo la kuliombea taifa ili Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29 mwaka huu ufanyike kwa amani na utulivu.
Mratibu wa Umoja wa Machifu wa mikoa ya Kusini, Chifu Sad Wabu (Mitondo wa Pili) ameyasema hayo wakati wa mkutano na wandishi wa habari kuhusu maandalizi ya matembezi hayo pamoja na shughuli zingine zitakazofanywa na viongozi hao.
Amesema matembezi hayo yanaratibiwa kwa ushirikiano kati ya Umoja wa Machifu na Taasisi isiyokuwa ya kiserikali ya Akida Wabu Development Foundation na yanatarajiwa kufanyika Oktoba 13 mkoani Mbeya na kwamba yatatanguliwa na mafunzo ya uongozi ya siku tatu kuanzia Oktoba 9 hadi Oktoba 12 mwaka huu.
Chifu Mitondo ambaye ni chifu wa Himaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, amesema machifu hao wanatoka katika mikoa tisa ya kusini ambayo ni Morogoro, Lindi, Mtwara, Ruvuma, Iringa, Njombe, Mbeya, Songwe na Rukwa.
Amewataka watanzania wote kuhakikisha wanalinda amani ya nchi kuelekea uchaguzi mkuu akidai kuwa endapo machafuko yatatokea hakuna Tanzania nyingine ya kukimbilia.
“Sisi machifu hatutaki taifa letu litumbukie kwenye machafuko kwa sababu tunaamini kwamba ikitokea hivyo sisi sote tutaathirika, hatuna Tanzania nyingine Zaidi ya hii tunayoishi, kwahiyo tunawaomba watanzania wote kuilinda amani hii,” amesema Chifu Mitondo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED