Hatma ya Mpina kugombea Urais kujulikana kesho

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 03:26 PM Sep 21 2025
Luhaga Mpina
PICHA: MPIGAPICHA WETU
Luhaga Mpina

MAHAKAMA Kuu ya Tanzania Masjala Kuu Dodoma, kesho itasikiliza shauri la kikatiba namba 20027 la mwaka 2025 la kuhoji uhalali wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kumuondoa Mgombea urais wa ACT Wazalendo, Luhaga Mpina kugombea nafasi hiyo.

Shauri hilo linasikilizwa mbele ya Majaji watatu Jaji Sylvester Kainda, Jaji Fredrick Manyanda, na Jaji Abdallah Gonzi. Aidha, kesho hiyo hiyo majira ya asubuhi Mahakama Kuu Masjala Kuu ya Dodoma, mbele ya Jaji Wilbert Chuma itaendelea kusikiliza na kutolea uamuzi mdogo shauri na. 23617 la mwaka 2025 juu ya kupinga uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa Tanzania ambao ulitumiwa na Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi-INEC kumuondoa Mpina kwenye orodha ya wagombea urais.
Shauri hilo linakuja kesho baada ya kuwasilishwa mahakamani kwa maombi ya hati ya dharura na kusikilizwa Septemba 16, 2025 na kutoa amri za:Wajibu maombi kuwasilisha majibu yao mpaka Septemba 18, mwaka huu, waleta maombi kuwasilisha majibu Septemba 19, 2025 na Septemba  22, 2025 mahakama imepanga kusikiliza ufafanuzi zaidi wa hoja zilizowasilishwa na itapangiwa siku ya kutoa uamuzi mdogo.
“Wakati tukiendelea na hatua za kisheria katika hili, tunawataka wagombea wetu wote kuendelea na kampeni za uchaguzi katika maeneo yao,”ilisema taarifa hiyo iliyotolewa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Chama ACT Wazalendo.