KATIBU Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Profesa Godius Kahyarara amewahakikishia wafanyabiashara na wawekezaji nchini Nigeria kuwa Rais Samia Suluhu Hassan anadhamira ya kuungamanisha uchumi wa Tanzania na Bara zima la Afrika.
Akizungumza leo kwenye kongamano la wafanyabiashara wa Nigeria na Tanzania katika Jiji la Lagos Nigeria mara baada ya kuanza safari za moja kwa moja kutoka Dar es Salaam mpaka Lagos Nigeria, amesema ni hatua ya Rais Samia kuekeleza dhamira ya kufungua fursa adhimu za kiuchumi.
Profesa Kahyarara alisema kwa sasa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) linahudumia soko la watu milioni 400 katika nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na Afrika Mashariki (EAC). “Kuanza kwa Safari za Lagos ni hatua kuelekea kufungamanisha Tanzania na soko lingine kubwa la Afrika Magharibi ambalo nalo lina watu takriban 400 na Nigeria peke yake ina watu zaidi ya milioni 200,”amesisitiza.
Aidha, amesema mkakati wa Serikali ya Tanzania ni kuanza safari za Accra muda wowote kuanzia sasa kama njia ya kuungamanisha soko la pamoja Afrika.
Naye, Waziri wa Usafiri wa Anga Nigeria, Festus Kayemo amewahakikishia washiriki wa kongamano hilo kuwa Serikali ya Nigeria inathamini mageuzi makubwa yanayoganywa na Tanzania na itaitumia fursa hiyo kuimarisha ushirikiano kwenye utalii, uchumi biashara madini na maeneo yote yatakayowezekana.
“Wafanyabiaahara na wawakilishi wao Nigeria wamepongeza hatua hii muhimu na kuomba suala la Visa rejea kwa wanaigeria wanaotaka kuingia Tanzania kuangaliwa, ili kuondoa kikwazo hicho,”amesema.
Akizungumza mwishoni mwa wiki wakati wa uzinduzi wa safari, Katibu Mkuu huyo amesema uchumi mkubwa wa Nigeria umeivutia Tanzania kuanzisha safari za ndege za moja kwa moja kutoka Dar es Salaam hadi Lagos.
Amesema Tanzania imeona matokeo makubwa baada ya kufungua biashara ya Afrika Kusini kupitia usafiri wa anga, na sasa inaangazia masoko mengine.
"Kwanini Lagos ni kwasababu ya uchumi mkubwa wa Nigeria, ni nchi ya pili kwa uchumi mkubwa Afrika, lakini kuna vipimo vingine Nigeria inakuwa iko juu ya Afrika Kusini kiuchumi,"amefafanua Profesa Kahyarara.
"Lakini tumeona matokeo makubwa ya kwenda Afrika Kusini, kwa hivi sasa Tanzania inafanya biashara sana na Afrika Kusini kuliko nchi za Afrika Mashariki,tunaimani kuna fursa kubwa kufungua uchumi na biashara,"amesema.
Prof. Kahyarara alisema pia kuna fursa za wawekezaji wakubwa na ukuaji wa sekta ya utalii ambapo Afrika Kusini na Nigeria zinashindana kwa kuwa na watalii wengi.
"Afrika Kusini tumetumia fursa,tukiongeza na Nigeria itaongeza sana soko la watalii hasa ndani ya Bara la Afrika na itaongeza uimara kuliko kutengemea masoko ya mbali.Huu ni mkakati wa kiuchumi,"amesema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED