Doyo: Serikali yangu itatoa ruzuku kwa wakulima wa miti

By Thobias Mwanakatwe , Nipashe Jumapili
Published at 05:05 PM Oct 05 2025
Doyo: Serikali yangu itatoa ruzuku kwa wakulima wa miti
PICHA: THOBIAS MWANAKATWE
Doyo: Serikali yangu itatoa ruzuku kwa wakulima wa miti

Mgombea urais kupitia Chama cha National League for Democracy (NLD), Doyo Hassan Doyo, amesema iwapo wananchi watampa ridhaa ya kuwa rais serikali yake itatoa ruzuku maalum kwa wakulima wa miti ili kuwawezesha kuendeleza kilimo hicho ambacho kinahitaji muda mrefu na mtaji mkubwa.



Akizungumza leo (Oktoba 4, 2025) na wananchi katika mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye viwanja vya soko la wakulima Njombe Mjini, amesema anafahamu changamoto kubwa zinazowakabili wakulima wa miti ya mbao, ikiwemo gharama kubwa za uzalishaji na muda mrefu wa kuvuna.

Doyo amesema kutokana na changamoto hiyo serikali yake itatoa ruzuku kuhakikisha kilimo hicho kinaendelea kwa tija na kuwa chanzo cha mapato ya uhakika kwa wananchi wa Njombe.

Aidha, Doyo aligusia umuhimu wa kuanzishwa kwa viwanda vya mbao mkoani Njombe akibainisha kuwa vitasaidia kuongeza thamani ya mazao hayo na kutoa ajira kwa vijana wengi akisistiza kuwa kupitia viwanda hivyo vya mbao zitapatikana fenicha bora zinazozalishwa hapa nchini. 

Amesema Serikali yake pia itanunua fenicha kutoka viwanda vya Njombe badala ya kuagiza kutoka nje ya nchi. “Tunataka fedha za Watanzania zibaki nchini na kuinua uchumi wa wakulima wetu,” alisisitiza  Doyo.