AJALI, ajali, ajali. Huo ulikuwa sawa na wimbo uliochukua chati ya juu kwa mwaka 2024 kutokana na matukio ya ajali yaliyotokea katika maeneo mbalimbali nchini.
Januari hadi Desemba kumekuwa na matukio hayo ambayo yamesababisha mamia ya watu kupoteza maisha, wengine kujeruhiwa na baadhi yao kupata ulemavu wa kudumu sambamba na upotevu wa mali na uharibifu wa vyombo vya moto. Kwa jumla, hakuna mkoa ambao haujaguswa na matukio ya ajali katika mwaka 2024.
Wakati zikiwa zimebaki siku chache kutamatika kwa mwaka 2024, matukio kama hayo yametokea wakati Watanzania wakiwa katika shamrashamra za Krismasi.
Desemba 24, mwaka huu, watu 11 walifariki dunia papo hapo na wengine 13 kujeruhiwa katika wilaya ya Handeni mkoani Tanga, ajali iliyohusisha gari la mizigo Mitsubishi Fuso lililokuwa likitoka Lushoto kwenda Dar es Salaam na Toyota Coster ikitoka Handeni kwenda Tanga mjini.
Ajali hiyo ikiwa haijatoka katika akili za Watanzania, Desemba 26 ikatokea ajali nyingine Tarakea, Rombo mkoani Kilimanjaro iliyohusisha basi la kampuni ya Ngasere na Toyota Noah. Katika ajali hiyo, watu 10 walipoteza maisha na wengine kujeruhiwa.
Tangu kuanza kwa mwaka huu, ajali zimekuwa jambo la kawaida licha ya serikali kupitia Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, kuwaonya madereva kwa kushindwa kufuata na kuheshimu sheria za usalama barabarani. Rais Samia Suluhu Hassan na viongozi wengine wakuu wa kitaifa wamekuwa mara kwa mara wakitoa maagizo kuhusu udhibiti wa ajali lakini maagizo hayo yamekuwa kama sikio la kufa.
VIFO 102 KANDA YA ZIWA
Katika kanda ya Ziwa, ajali zilizoripotiwa kuanzia Januari mpaka jana, zilisababisha vifo 102 huku ajali za barabarani zikiongoza kwa kusababisha vifo 82.
Jinamizi la ajali katika ukanda huo, lilianzia Januari 13, baada ya watu 22 kufukiwa na kifusi na kufariki dunia. Hatua hiyo ilisababisha Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, kutangaza kufunga machimbo hayo na kuwataka wachimbaji kuunda vikundi ili visajiliwe wizarani.
Januari 30, katika Manispaa ya Shinyanga, Daudi Mwandu (25) mkazi wa Bugweto aligongwa na gari aina ya Toyota Land Cruiser lenye namba za usajili T. 952 BSP na kufariki dunia huku abiria wake, Mtatiro Wambura (33), akijeruhiwa.
Baada ya ajali hiyo wananchi waliandamana kutaka udhibiti wa kasi za madereva na kulishinikiza Jeshi la Polisi kumkamata dereva wa gari hilo aliyekimbia na gari. Kamanda wa Polisi mkoani humo, Janeth Magomi, alifika katika eneo la tukio kutuliza hasira za wananchi na kuwasihi kwamba serikali imesikia kilio chao.
Mkoani Kagera, ajali ya basi la shule binafsi ya Kemebos ilisababisha kifo cha mwanafunzi kidato cha tano, Frank Makage, na wengine kujeruhiwa lilipokuwa likisafirisha wanafunzi kwenda likizo.
Aprili 24, mkoani Mwanza katika eneo la Daraja la Mwananchi, majira ya saa 1;20 asubuhi, gari lenye namba za usajili T 744 DCG Toyota Hiace lililokuwa limebeba wanafunzi wa Shule ya Msingi Mchepuo wa Kiingereza Nyanza, lilifeli breki na kusababisha kifo cha mtu mmoja huku wengine watano wakijeruhiwa.
Ajali nyingine ilitokea Juni 27, majira ya saa 12:15 jioni wilayani Chato, mkoani Geita ambayo ilisababisha watumishi wawili wa afya kupoteza maisha baada ya kugongwa na gari aina ya Toyota Probox wakiwa kwenye pikipiki wakitoka kwenye njia ndogo kuingia kwenye barabara kubwa pasipo kuchukua tahadhari.
Ajali nyingine iliyotokea huko mkoani Simiyu ilisababisha vifo vya watu watatu wa familia moja na ng'ombe sita ikihusisha basi la kampuni ya Ally's na Mitsubishi Fuso.Taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Edith Swebe, ilitaja chanzo cha ajali hiyo iliyotokea katika Kijiji cha Ruguru wilayani Itilima kuwa ni mwendokasi na dereva wa Fuso aliyejaribu kupishana na magari bila kuchukua tahadhari.
Wilayani Kahama, mkoani Shinyanga, lori lenye namba za usajili T.854 DBY na tela namba T.180 DVH liligongana na gari lenye namba T.195 EEY na tela namba T.811 SYU lililokuwa likitokea Bukoba na mzigo wa kahawa na kuwaka moto na kusababisha vifo vya watu watatu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga Janeth Magomi alisema chanzo cha ajali hiyo ni lori lililokuwa likiendeshwa na Rajab Tabu likilikwepa gari la mchanga bila kuchukua tahadhari.
Basi la Kampuni ya Nyehunge likitokea Morogoro kwenda Mwanza, liliacha njia na kugongana na basi la Asante Rabi lililokuwa likitokea Mwanza kwenda Arusha katika eneo la Ukiruguru wilayani Misungwi na kusababisha vifo vya watu wanane huku 39 wakijeruhiwa.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Naibu Kamishna (DCP) Wilbroad Mutafungwa, alisema chanzo chake ni mwendo kasi na dereva kuchepuka bila kuchukua tahadhari.
Wilayani Tarime, mkoani Mara Daniel Elias, na mke wake, Kadogo Daniel, walifariki dunia kwa nyakati tofauti baada ya kugongwa na lori lililokuwa katika mwendokasi wakiwa katika pikipiki kisha lori hilo kutokomea nchini Kenya.
Aidha, wilayani Bunda mkoani Mara, watu wanne walifariki dunia baada ya lori aina ya Mitsubishi Fuso lililokuwa limebeba mawe, kuacha njia na kuparamia wananchi na wafanyabiashara katika eneo la mataa kuacha njia na kugonga gereji
Katika wilaya ya Karagwe mkoani Kagera, lori la mizigo aina ya Scania, liligongana na Toyota Hiace pamoja na Toyota Coaster katika eneo la Kihanga na kusababisha vifo vya watu saba na wengine tisa kujeruhiwa.
Kamanda wa Polisi mkoani humo Blasius Chatanda, alisema chanzo ni uzembe wa dereva wa lori kutochukua tahadhari na kuendesha gari kwa mwendo kasi.
Desemba 21, Kagera katika wilaya ya Biharamulo, basi la abiria Kampuni ya Capco One lilifeli breki katika mteremko na kusababisha vifo vya watu 11 huku wengine 42 wakijeruhiwa.
TABORA NAKO
Juni 19 mkoani Tabora, basi la kampuni ya Mumuki liligongana na gari ndogo aina ya Toyota Hiace. Katika ajali hiyo, watu wawili, akiwamo Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Wilaya ya Igunga, Zawadi Wiliam (60) walifariki dunia na wengine 12 walijeruhiwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Richard Abwao, alisema ajali hiyo iliyotokea saa 7:00 mchana, ilisababishwa na dereva Richard Gabriel (42) aliyekuwa akijaribu kuyapita magari mengine matatu bila kuchukua tahadhari.Ajali nyingine mkoani humo ilihusisha gari la abiria aina ya Toyota Hiace lililogongana na Mitsubishi Fuso. Katika ajali hiyo, watu 14 wakiwamo vichanga wawili walifariki dunia na wengine tisa walijeruhiwa.
Kamanda Abwao alisema chanzo cha ajali hiyo ni dereva kutaka kuchepuka na kujaribu kuyapita magari mengine akiwa kwenye mwendokasi.
AJALI MBEYA
Juni 5, ilitokea ajali mbaya katika Mteremko wa Mbembela jijini Mbeya baada ya lori aina ya Scania lililokuwa limebeba shehena ya kokoto likitokea Uyole kwenda Tunduma kufeli breki na kuyaparamia magari mawili, pikipiki na guta, hivyo kusababisha vifo vya watu 13 papo hapo na kujeruhi 18.
Lori hilo lilianza kuigonga gari ndogo aina ya Harrier yenye namba za usajili T. 120 DEL na kupoteza mwelekeo kwenda kuligonga gari aina ya Toyota Coaster lililokuwa likitoka Tunduma kwenda jijini Mbeya.
Ajali ya pili ilitokea katika Kijiji cha Itamboleo Kata ya Chimala wilayani Mbarali. Basi la Kampuni ya Shari Line lenye namba za usajili T. 896 DHK lililokuwa likitokea mkoani Rukwa kwenda Njombe, liliacha njia na kugonga gema kisha kuanguka.
Ajali hiyo ilisababisha vifo vya watu tisa na kujeruhi 18. Chanzo cha ajali kilielezwa kuwa ni uzembe wa dereva aliyekuwa akiendesha basi hilo. Alikamatwa na polisi baada ya ajali hiyo na kuchukuliwa hatua.
Septemba 6, ajali nyingine ilitokea katika Kijiji cha Lwanjilo, wilayani Mbeya ikihusisha basi la Kampuni ya AN CLASSIC lililokuwa likitokea Mbeya kwenda Tabora baada ya kuacha njia na kugonga gema kishakusababisha vifo vya watu 12 na kujeruhi wengine 36.
Ilibainika kuwa gari hilo lilikuwa limezimwa kidhibiti mwendo kwa zaidi ya mwezi hali iliyokuwa inasababisha madereva kuendesha kwa mwendokasi bila kudhibitiwa.
Ajali nyingine iliyogharimu maisha ya watu ilitokea Septemba 27, ambapo gari aina ya fuso lililokuwa limebeba abiria likitokea katika Mji wa Mbalizi kwenda kwenye Mnada wa Ilembo lilifeli breki na kupinduka katika Kijiji cha Jojo. Watu 12 walifariki dunia na 23 walijeruhiwa.
DODOMA PIA
Ajali ya gari iliyogonga treni ilisababisha vifo vya mume na mke katika makutano ya reli na barabara eneo la Medeli, jijini Dodoma huku binti yao wa miaka miwili aliyekuwapo kwenye gari hilo akinusurika.
Wanandoa hao, Mhandisi Hussein Chilala na Furaha Hamisi walipata ajali baada ya kugonga treni iliyokuwa inakwenda mikoa ya Tabora na Kigoma. Ajali hiyo ilitokea majira ya saa 2:00 usiku wa Aprili 4, 2024 wakati wanandoa hao wakienda kununua keki kwa ajili ya kumbukizi ya siku ya kuzaliwa ya binti yao.
Ajali nyingine ilitokea Desemba 7, 2024 katika eneo la Chinangali One, Barabara Kuu ya Dodoma-Morogoro, baada ya malori matatu kugongana na kusababisha msongamano mkubwa wa magari pamoja na madhara kwa vyombo vya usafiri vilivyohusika.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio, ajali hiyo ilihusisha malori matatu yaliyokuwa yakisafiri kwa kasi, moja liligongana na magari mengine yaliyokuwa yakiendelea na safari zao.
Aidha, zaidi ya wabunge 50 waliokuwa wakisafiri kwa basi kutoka Dodoma kwenda Kenya kushiriki michezo walipata ajali eneo la Mbande mkoani Dodoma. Wabunge kadhaa walipata majeraha ya mwili kutokana na ajali hiyo.
Basi hilo la Bunge likiwa katika mwendo wa kawaida lilikutana na changamoto ya gari lingine lililokuwa limeangusha mizigo barabarani na wakati dereva akijaribu kukwepa mizigo hiyo, ndipo basi hilo lilipoacha njia na kuingia porini.
Miongoni mwa wabunge waliojeruhiwa ni pamoja na Jackson Kiswaga (Kalenga) Jesca Msambatavangu (Iringa Mjini) na wa Viti Maalum, Grace Tendega
AJALI ZINGINE
Katika mwaka huu pia, kulitokea ajali zingine ikiwamo ya boti ya mizigo Septemba 25, katika Ziwa Victoria eneo la Kirumba na kusababisha vifo vya watu tisa.
Ajali nyingine ilitokea Itilima mkoani Simiyu ikihusisha mabinti wanne waliofariki dunia baada ya kuzama kwenye dimbwi lililochimbwa kwenye makazi ya watu kwa ajili ya uchimbaji madini walipokwenda kufua na kuchota maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.
Watoto hao ni wa familia tatu tofauti ikiwa kati yao wawili ni wa familia mmoja na watatu ni wanafunzi wa Shule ya Sekondari Lagangabilili walifariki dunia baada ya mwenzao kuteleza na kuzama katika dimbwi hilo na wao kuanza kujaribu kumwokoa.
Mkoani Tabora, mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi minane, Martin Ndalu, alifariki dunia na mwingine kujeruhiwa baada ya kupigwa na shoti kupitia waya uliokuwa ukishikilia nguzo ya umeme katika kata ya Kitete, Manispaa ya Tabora.
Katika mkoa wa Mwanza, watu wawili walifariki dunia kwa kupigwa na mshituko wa umeme 'shot' wakati wakihamisha nguzo kutoka kwenye Mradi wa ujenzi wa barabara jijini Mwanza.
Kamanda Mutafungwa alisema tukio lilitokea Agosti 10, 2024 majira ya saa 7:30 mchana katika Mtaa wa Semba wilayani Nyamagana.
Mkoani Kagera, watoto wawili wa familia moja, Justa John (9) aliyekuwa mwanafunzi wa darasa la kwanza Shule ya Msingi Mubembe na Julietha John (4) wa Kitongoji Mubembe, Kijiji cha Lwagati wilaya ya Bukoba, walifariki dunia katika ajili ya moto baada ya nyumba walimokuwa wakiishi kuwaka na kuteketea.
Wilayani Nzega, mkoani Kagera watu watatu wamefariki dunia kwa kuangukiwa na ukuta wa nyumba na kusababisha vifo katika kijiji cha Iyombo Nyasa kata ya Utwigu.
Kamanda Abwao aliwataja marehemu hao kuwa ni Rashidi Matoma, Chiku Mihayo na Hamisi Rashid. Alisema watu hao walifariki dunia baada ya kuangukiwa na ukuta ambao ulijengwa kwa matofali ya tope katika chumba walichokuwa wamelala wakati wa usiku.
Imeandaliwa na Vitus Audax (MWANZA), Nebart Msokwa (MBEYA) na Pul Mabeja (DODOMA).
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED