MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu, Yanga leo watashuka kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam kucheza mechi ya mwisho ya Ligi Kuu kwa mwaka huu huku wakiahidi kuwapa wanachama na mashabiki wa timu hiyo zawadi ya ushindi kwa ajili ya kuuaga mwaka 2024.
Nahodha ya timu huyo, Bakari Mwanyeto amewataka wanachama na mashabiki wa Yanga kumiminika uwanjani kwa wingi ili kuwapa sapoti ya kuwashangilia na wao watawapa zawadi ya ushindi ili washerehekee vyema kuuaga mwaka huu.
Yanga itacheza dhidi ya Fountain Gate katika mchezo ambao kama itashinda itafikisha pointi 39, ikimaliza mechi zake za mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kocha Mkuu wa timu hiyo, Sead Ramovic amesema kwa mara nyingine tena wanakwenda kucheza mchezo mgumu, lakini kupambana na kujituma kwao ndiko kunaweza kuwapa ushindi kwenye mchezo huo.
"Tunakwenda kucheza mechi nyingine ngumu, tunataka kuonyesha watu nini tunafanya, nimesoma timu pinzani ni nzuri, ila kwa sasa tunajiangalia sisi nini tutakwenda kuoonyesha uwanjani kwa ajili ya kushinda na kupata pointi tatu.
Tunajua wanakuja na mfumo wa kukaa nyuma na kutushambulia kwa kushtukiza kitu ambacho ni hatari, lakini kujituma na nidhamu ndiyo kitu pekee ambacho kinaweza kutupa ushindi leo, tunataka kuitawala mechi," alisema kocha huyo.
Mwamnyeto, alisema kazi kubwa watakayoifanya leo upande wa mabeki ni kuhakikisha washambuliaji wao hatari hawagusi nyavu zao.
"Tunajua Fountain Gate ni moja kati ya timu zenye safu kali ya ushambuliaji, kwa hiyo mimi na mabeki wengu tunakwenda kufanya kazi ya kuwazuia ili wasilete madhara, ikiwezekana wasiguse nyavu zetu.
Fountain Gate ina mastraika, Selemani Mwalimu mwenye mabao sita, na Edgar William ambaye ana mabao matano.
Timu hiyo kwa sasa inashika nafasi ya nne kwenye Ligi Kuu kwa kufunga mabao mengi zaidi. Simba ikiongoza kwa mabao 30, Yanga mabao 27, Azam ikiwa imefikisha 25, Fountaig Gate ikiwa na mabao 24.
Kocha wa timu hiyo, Mohamed Muya, amekiri kuwa wanakwenda kucheza mechi ngumu dhidi ya timu bora ya Yanga, lakini haiwaondolei ari ya kupambana ili kupata ushindi.
"Tunaiheshimu Yanga, ni moja kati ya timu nzuri na kubwa kwenye nchi hii ambazo zimekuwa na mwendelezo mzuri, imesajili vizuri, lakini ni wakati wetu sasa timu za madaraja ya kati kuonyesha tumekua kiasi gani, tunapokwenda kumkabili adui tunaangalia nguvu yake na mapungufu yake, tumeiangalia, tumewapa mbinu wachezaji wetu wa kuikabili," alisema kocha huyo.
Fountain Gate kwa sasa ipo nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikikusanya pointi 20.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED