MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imekitaja Chuo Kikuu Mzumbe (MU) kilichoko mkoani Morogoro kuwa kinara katika ulipaji wa kodi kwa kipindi cha Julai hadi Novemba, 2024.
Pongezi hizo zilitolewa juzi na Mkurugenzi wa Utafiti na Sera wa TRA, Dk. Ephraim Mdee, mjini hapa wakati wa kukabidhi cheti cha pongezi na kutambua mchango wa chuo kikuu hicho katika ulipaji wa kodi.
Dk. Mdee alisema mamlaka hiyo inatambua na kuthamini taasisi zinazolipa kodi ya serikali kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizopo.
"Nachukua nafasi hii kukipongeza sana Chuo Kikuu Mzumbe. Mmekuwa kinara katika ulipaji wa kodi. Tunashirikiana nanyi na mmekuwa mstari wa mbele katika hili,” alisema.
Dk. Mdee alisema Desemba kila mwaka, TRA imekuwa ikifanya matendo ya kutoa shukrani kwa walipakodi wazuri nchini kwa kutambua mchango wao na kuwapatia vyeti nchini kote .
Alisema mkoa wa Morogoro umefanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato na unaendelea kufanya vizuri.
Dk. Mdee alisema miezi mitano iliyopita kufikia Novemba 2024, mamlaka hiyo mkoani Morogoro ilifikia lengo la asilimia 102 na kutokana na ushirikiano unaooneshwa na walipakodi.
Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu hicho, Prof. Allen Mushi, alisema Mzumbe imejikita katika kufundisha masuala ya uongozi, fedha, sheria na biashara, hivyo ni lazima yanayofundishwa darasani yaendane na vitendo .
"Yale tunayofundisha darasani yanaendana na vitendo. Tunawafundisha wanafunzi wetu masuala ya uongozi, uwajibikaji, nidhamu, haki na wajibu," alisisitiza Prof. Mushi.
Mbali na chuo hicho, viongozi wa mamlaka hiyo waliwatembelea wafanyabishara kadhaa wakiwamo wa Soko la Chifu Kingalu, Manispaa ya Morogoro.
Baadhi ya wafanyabiashara, akiwemo Mwenyekiti wa Machinga Mkoa wa Morogoro, Faustine Francis, waliishauri mamlaka hiyo kupanua wigo wa utoaji wa elimu ya kodi kwa wananchi na wafanyabiashara walioko maeneo yanayokua kibiashara.
Mwenyekiti huyo alisema lengo ni kuwawezesha wawe na uelewa zaidi na ili hatimaye waone umuhimu kwao kulipa kodi kwa hiari kwa ajili ya maendeleo endelevu ya Watanzania wote .
Mamlaka hiyo imesogeza huduma kwa wafanyabiashara na kuweka vituo vya utoaji wa namba ya mlipakodi (TIN) na namba ya malipo ya kodi kwenye Soko Kuu la Chifu Kingalu na ofisi ya Kata ya Kihonda, Manispaa ya Morogoro.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED