TAASISi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imefungua tawi jipya ikiwa ni kituo cha nne cha tiba Dar es Salaam, kwa taasisi hiyo, kutoa fursa kwa wananchi kupata huduma za matibabu karibu na wanakoishi.
Kituo kikuu cha matibabu hayo ni JKCI-Upanga; JKCI-Dar Group; JKCI-Kawe (Mkapa Health Plaza) pamoja na JKCI-Oyster Plaza, vyote vikiwa mkoani Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk. Peter Kisenge, akizungumza na waandishi wa habari jana, jijini Dar es Salaam, kwenye ufunguzi wa tawi la JKCI-Oyster Plaza, Oysterbay, wilayani Kinondoni, Dar es Salaam.
Alisema taasisi hiyo imekuwa ikiwafikia wananchi walipo pamoja na mikoani, kuwapa huduma bobezi za uchunguzi na matibabu ya moyo.
Alisema tawi la JKCI-Oyster Plaza, limeanza kutoa huduma bobezi za moyo mwishoni mwa wiki, lengo ni kuwapa fursa wananchi kupata huduma katika maeneo tofauti na kupunguza msongamano ulioko katika makao makuu ya taasisi, Upanga.
“Tumekuwa tukiwafuata wananchi mikoani kuwapa huduma sasa tumeamua kuanzisha matawi ya Taasisi, hii pia ni sehemu ya kuwafuata wananchi mahali walipo, kwani hapa tulipo leo (juzi), tunawapa nafasi wananchi wa eneo hili kupata huduma karibu, lakini pia hata wale wanaotoka mbali tunawapa nafasi, ili kupunguza msongamano uliopo makao makuu,” alisema Dk. Kisenge
Dk. Kisenge, ambaye pia ni bingwa wa magonjwa ya moyo, alisema JKCI pia inaendelea kuyafikia makundi ya watu mbalimbali kuwapa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo, ili yote kuwa mabalozi wazuri kwa wenzao na kuwa na tabia za kuchunguza afya zao mara kwa mara.
“Tumekuwa tukiwafikia watu tofauti kuwafanyia uchunguzi wa magonjwa ya moyo, kipindi hiki cha kufunga mwaka tunatoa huduma kwa wasanii na wanamichezo kila Jumamosi na Jumapili katika kliniki yetu ya Kawe, wanahabari tulishawapa huduma hii huko nyuma ila tutakuja kuwarudia tena.”
Alitoa wito kwa wasanii na wanamichezo kuendelea kujitokeza kufanya uchunguzi wa magonjwa ya moyo, akisema kinga ni bora kuliko tiba na kama watagundulika mapema watakuwa kwenye nafasi ya kutibiwa magonjwa hayo mapema na kupona.
Miongoni mwa wananchi waliofika katika tawi hilo jipya, ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alisema huduma za afya zikiwa karibu na jamii zinatoa motisha kwa jamii kufika hospitali na kufanya uchunguzi wa afya hivyo kupunguza matumizi ya dawa yasiyo sahihi.
“Mara nyingi tumekuwa tukipata hali za maumivu ama kuumwa kichwa, mafua, kikohozi, kifua tunaenda duka la dawa kununua dawa tu bila ya kufanya uchunguzi lakini kama tutakuwa karibu na hospitali itatusaidia kwenda kupima kwanza na kupata ushauri wa daktari kabla ya kununua dawa,” alisema.
Msimamizi wa kliniki JKCI-Oyster Plaza, Nyanjura Nyaruga, alisema kliniki hiyo imeanza kwa kuwa na mwitikio mkubwa wa watu waliofika kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo.
Nyanjura ambaye pia ni Ofisa Muuguzi Mbobezi wa Magonjwa ya Moyo, alisema katika kliniki hiyo wanatoa huduma za kliniki ya moyo; kliniki ya mishipa ya damu; kliniki ya magonjwa ya moyo kwa watoto; huduma za maabara, huduma za mazoezi (fiziotherapia) kwa wagonjwa wa moyo na huduma za dharura.
“Wananchi wasisite kufika katika kliniki yetu hii kwani tumejipanga kufikisha huduma bora kwenu na tutakuwa tukitoa huduma zetu kwa muda wa saa 24,” alisema Nyanjura.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED