Mwinyi atangaza neema mikopo elimu ya juu

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 01:54 PM Dec 29 2024
Rais wa Zanzibar, Dk, Hussein Ali Mwinyi
Picha: Mtandao
Rais wa Zanzibar, Dk, Hussein Ali Mwinyi

RAIS wa Zanzibar, Dk, Hussein Ali Mwinyi, ameiagiza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kuhakikisha wanafunzi wote wenye sifa wanapatiwa ili kuendelea na elimu ya juu kwa wakati.

Dk.  Mwinyi ambaye ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA) alisema hayo jana alipowatunuku vyeti wahitimu wa ngazi mbalimbali katika mahafali ya 20 ya chuo hicho yaliyofanyika katika ukumbi wa Dk. Ali Mohamed Shein, Tunguu, Wilaya ya Kati mkoa wa Kusini Unguja.

Dk, Mwinyi alisema kwa kutambua umuhimu wa elimu, serikali itaendelea kuchukua kila juhudi kuhakikisha mazingira bora ya upatikanaji wa elimu kwa ngazi zote ili kuwa na wana taaluma wenye weledi , ujuzi utakaochochea maendeleo na ukuaji wa uchumi.

Rais Dk, Mwinyi alieleza kufarijika na ongezeko la wahitimu wa chuo hicho kila mwaka hatua inayoakisi dhamira ya chuo ya kuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi.

Alisema kumekuwa na ongezeko la asilimia 8.4 la wahitimu mwaka 2023/24  kwa wahitimu 2,291 kulinganisha na wahitimu 2,101 mwaka uliopita pamoja na ongezeko la wahitimu wanawake kwa asilimia 61 na kuwataka kuwa sehemu ya mabadiliko chanya kwenye maendeleo ya jamii .

Dk, Mwinyi alisema serikali imetenga Sh. bilioni 33.4 kwa ajili ya mikopo na wanafunzi 8.870 wanaotarajiwa kupatiwa mikopo hiyo.

Aidha, alisema serikali itaendelea kuandaa programu mbalimbali katika taasisi za kitaaluma za ndani ya nchi na kimataifa ili kuinua kiwango cha taaluma kwa wataalamu ,wafanyakazi na wanataaluma wa SUZA ili kuongeza hadhi ya chuo na kuwa chenye kutoa elimu bora.  

Alisisitiza kuwa lengo ni kuwa na chuo kinachotoa wahitimu wenye sifa, weledi na ujuzi watakaohimili ushindani katika soko la ajira au kujiajiri na kuendana na kasi ya maendeleo iliyopo hivi sasa 

Dk. Mwinyi alibainisha kuwa serikali imejikita katika kuimarisha ubora wa elimu kwa kutoa mafunzo endelevu kwa wanataaluma na watumishi waendeshaji wa SUZA kwa kushirikiana na taasisi za kimataifa ili kuleta programu bora na zinazokidhi viwango vya kimataifa.

Alilipongeza Baraza la Chuo hicho kwa kufundisha shahada ya sayansi ya utabibu ya kinywa na meno na kuanzisha programu zingine mpya nne za elimu chuoni hapo zikiwamo Shahada ya Elimu Jumuishi na Mahitaji Maalum ya Kielimu, Shahada ya Elimu ya Amali na Shahada ya Elimu na Lugha pamoja Shahada ya Mafunzo ya Ubaharia inayotarajiwa kuanza kufundishwa mwaka 2025.

Rais Dk, Mwinyi alisema hatua hiyo itaiwezesha serikali kuwa na wataalamu wa kutosha katika sekta mbalimbali watakaotoa mchango wao katika Maendeleo ya kijamii.

Aidha, Rais Dk, Mwinyi alimtunuku Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais ,Katiba, Sheria ,Utumishi na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman, Shahada ya Heshima ya Udaktari wa Falsafa ya Elimu ya Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA).

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Lela Moh'd Mussa, alisema chuo hicho kimekuwa alama maalum ya utambulisho wa Zanzibar kitaaluma kwa mafanikio ya kutoa wahitimu na taaluma bora.

Alieleza fursa ya kuwapo kwa mikopo kwa wanafunzi wa ngazi ya diploma kumeongeza idadi ya wanafunzi kujiunga na chuo hicho kwa ngazi hiyo na kuahidi wizara hiyo kuhakikisha chuo kinaimarika na kupata hadhi kimataifa.

 Makamu Mkuu wa SUZA, Prof. Makame Haji, alisema mipango bora ya serikali na miongozo, busara na hekima za Rais Dk. Mwinyi zimekuwa kichocheo cha mabadiliko na maendeleo makubwa ya chuo hicho.

Alisema kutokana na ongezeko la wahitimu, chuo kina mpango kuendesha miradi tofauti ya upanuzi wa miundombinu ya majengo kwa kuwa na majengo ya ghorofa kupitia mpango wa mkuu wa chuo hicho. 

Hatua hiyo itaambatana na ujenzi wa maabara ya sayansi ,Skuli ya Kilimo, Skuli ya Elimu ya Lugha za Kigeni, ujenzi wa Skuli ya Afya, Sayansi na Tiba ikiwa miongoni mwa miradi   

Zaidi ya wahitimu 2,200 wa ngazi ya vyeti, stashahada, shahada, na shahada ya uzamili na uzamivu walitunukiwa vyeti vyao katika mahafali hayo.