Sita wafariki dunia gari likiwaka moto

By Gideon Mwakanosya , Nipashe Jumapili
Published at 02:02 PM Dec 29 2024
Watu sita wamefariki katika ajali ya gari aina ya Prado lenya namba T 647 CVR, iliyotokea mpakani mwa wilaya za Mbinga na Nyasa kwenye eneo la Chunya leo Desemba 28, 2024. Pichani maofisa na wa taasisi mbalimbali.
Picha: Mtandao
Watu sita wamefariki katika ajali ya gari aina ya Prado lenya namba T 647 CVR, iliyotokea mpakani mwa wilaya za Mbinga na Nyasa kwenye eneo la Chunya leo Desemba 28, 2024. Pichani maofisa na wa taasisi mbalimbali.

WATU sita wakiwamo walimu wanne wa Shule ya Msingi Lumalu, kata ya Upolo, Nyasa mkoani Ruvuma, wamefariki dunia baada ya gari walilokuwa wakisafiria kutoka katika cha kijiji Upolo kwenda Kilosa Mbambabay, kuungua moto.

Mkuu wa Wilaya ya Nyasa, Peres Magiri, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo jana saa 2:00 asubuhi katika eneo la kona za Chunya inapopita barabara inayotoka Mbinga - Mbambabay.

Alisema  watu hao walipata ajali wakiwa njiani kwenda  kwenye usaili wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC)  ya uandikishaji wa daftari la kudumu la wapigakura. Gari hilo aina ya Toyota Prado liliacha njia na kugonga gema la  barabara kisha kupinduka na kuwaka moto.

Mkuu huyo wa wilaya alisema kilichosababisha watu hao kushindwa kujiokoa na kuungua moto ni  milango ya gari hilo  kujifunga.

“Jitihada mbalimbali zilifanyika, kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ilikwenda kwenye eneo la tukio kuona namna ya kuondoa miili ya marehemu hao na kuisafirisha kwenda hospitali ya serikali ya wilaya ya Mbinga kwa ajili ya taratibu za kufanya uchunguzi wa vinasaba (DNA) ili miili ikabidhiwe kwa ndugu zao,” alisema.

Magiri aliwataja waliofariki dunia kuwa ni  dereva na mmiliki wa  gari hilo, Vincent Milinga,  na walimu Damas  Nambombe, Dominika Ndau, Judith Nyoni, Sylvester Mtuhi  na mfamasia  Boniface Mapunda.

Jitihada za kumpata Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Ruvuma, Marco Chilya, kuzungumzia suala hilo  ziligonga mwamba baada ya kupigiwa simu zaidi ya mara mbili  bila kupokewa.