RAIS Samia Suluhu Hassan, ametoa zawadi kwa watoto yatima na wenye mahitaji maalumu katika halamshauri za Msalala, Ushetu na Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga, kwa kuwapatia vitu vyenye thamani ya Sh. milioni saba.
Hatua hiyo ni kusherehekea mwaka mpya wa 2025, aidha ni utaratibu wa Rais Samia, kuwakumbuka yatima wanaoishi mazingira magumu, wajane pamoja na watu wenye ulemavu, huku akisisitiza wengine kuiga mfano huo.
Akikabidhi zawadi hizo katika moja ya Kituo cha Kulelea Watoto Yatima Mvuma, kilichopo kata ya Nyasubu, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha, alisema wamekumbukwa na Rais kwa kupewa mahitaji maalumu.
Alisema Rais Samia amekuwa na utaratibu huo kila mwaka, ikiwa ni sehemu ya kuwapatia faraja makundi hayo, ili na wao washerehekee sikukuu za mwisho wa mwaka kama yalivyo makundi mengine.
Chacha alitaja mahitaji yaliyokabidhiwa kwa makundi hayo kuwa ni pamoja na mafuta ya kupikia, sukari, mchele na mahitaji ya shule kwa watoto wanafunzi wanasoma shule za msingi na sekondari, yakiwamo madaftari na kalamu na kuwataka wenye uwezo kuyafikia makundi na kuyasaidia mahitaji muhimu.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama, Masoud Kibetu, aliwasihi wananchi na jamii kwa ujumla kuendelea na utaratibu kuwajali watoto hao wenye mahitaji, kwa kuwa wengi wameshindwa kutimiza ndoto zao za kielimu kwa kukosa mahitaji.
Msimamizi wa Kituo cha Mvuma, Laurine Noel, alisema mahitaji yaliyotolewa na Rais yatawasaidia kupunguza changamoto za ukosefu wa chakula kituoni na wale wanafunzi waliokuwa wanahitaji vifaa vya shule watasoma na kutimiza ndoto zao na wapo wanaofanya vema kwenye masomo.
Alisema watoto hao wamekuwa wakihitaji mahitaji mengi, zaidi ni chakula na kuwaangukia watu wenye uwezo kujitokeza na kuwasaidia, ili waondokane na kuomba msaada mara kadhaa na kwamba asilimia kubwa ya watoto wanaowalea ni wanaotelekezwa na ndugu, wakiwa bado ni wachanga.
"Tunapongeza Rais wetu Dk Samia kwa kuwakumbuka na kuwapatia mahitaji muhimu, kituo hiki kina jumla ya watoto 40 kati yake wasichana 27 na wavulana 14. Wanafunzi wanahitaji mahitaji, ili wasome na kutimiza ndoto zao,. Msaada huu nitahakikisha unawafikia watoto wote kwa usawa," aliongeza.
Mmoja wa wanufaika na zawadi hizo, Victoria Justine, alimpongeza rais kwa kuwakumbuka kila mwaka na kuwapatia mahitaji mbalimbali, vikiwamo vifaa vya shule na kumuahidi kusoma na kutimiza ndoto zao, ili kuja kuwasaidia wenzao.
Alisema wamekuwa wakijifunza kusoma kwa bidii baada ya kuwaona wenzao waliokuwa nao kwenye vituo kusoma mpaka vyuo vikuu, hivyo nao wanatamani kuwa kama wao na kwamba akimaliza masomo yake na kupata ajira, atakuwa anawasaidia watoto wanaotoka katika mazingira magumu.
Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mboni Mhita, alisema mahitaji yenye thamani ya Sh. milioni saba, yametolewa kwa watoto wanaoishi mazingira magumu na kulelewa katika vituo vya watoto, wajane, watu wenye ulemavu na wazee katika halmashauri za Msalala, Ushetu na Manispaa ya Kahama.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED