DC Kibaha kuzindua soko la kisasa Des 7

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 06:49 PM Dec 03 2024
Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Nickson John.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Nickson John.

Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Nickson John, anatarajiwa kuongoza wakazi wa mji wa Kibaha katika ufunguzi wa soko la kisasa la maduka (shopping mall) lililojengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 8.

Uzinduzi huo utafanyika Desemba 7, ukikamilika mbele ya kituo cha mabasi.Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha, Dk. Rogers Shemwelekwa, ameeleza hayo katika kikao cha kamati ya ushauri cha wilaya, akisisitiza kuwa wananchi wanapaswa kujitokeza kwa wingi kushiriki tukio hilo. 

Dk. Shemwelekwa amesema soko hilo litakuwa na bidhaa mbalimbali za kisasa, zikiwemo nguo ambazo mara nyingi zimekuwa zikiletwa jijini Dar es Salaam.

“Wananchi sasa wataweza kufanyia manunuzi karibu na majumbani mwao. Kuna maduka makubwa yenye nguo za kila aina, ambazo hata Kariakoo haziwezi kupatikana, na bei ni rafiki kwa jamii,” amesema.

DC, Nickson amesisitiza kuwa kikao cha kamati ya ushauri ni sehemu muhimu ya kupokea mawazo ya wananchi kwa ajili ya maendeleo ya wilaya, akitoa pongezi kwa Mkurugenzi wa Mji kwa usimamizi bora wa mapato, ambao umewezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo ununuzi wa madawati 4000 na kugawa shilingi milioni 10 kwa kila kata kuboresha miundombinu ya barabara.