MFUKO wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umeshiriki katika Maonesho yaliyoandaliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, pembezoni mwa Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Watu Wenye Ulemavu Duniani, katika ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam, Desemba 3, 2024, ambapo mgeni rasmi alikuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati,Dk. Doto Biteko.
Aidha maadhimisho hayo yamekwenda sanjari na Uzinduzi wa Mpango Kazi wa Taifa wa Haki na Ustawi kwa Watu wenye Ualbino na Mkakati wa Kitaifa wa Teknolojia Saidizi.
Kwa mujibu wa Meneja wa PSSSF, Kanda ya Ilala, Amina Kassim, PSSSF imeshiriki ili kuunga mkono juhudi za serikali katika kuinua ustawi wa makundi maalum lakini pia kutoa elimu ya hifadhi ya jamii na kutoa huduma.
“Moja ya jukumu la msingi la Mfuko ni ulipaji wa Mafao; Jumla ya Mafao saba (7) yanalipwa na PSSSF ambapo miongoni mwa mafao hayo ni Fao la Ulemavu.” amefafanua Amina.
Aidha, utoaji huduma kwa kutumia teknolojia, PSSSF Kidigitali, umesaidia sana kupunguza adha kwa wanachama hususan wenye ulemavu ambapo kwa sasa wanaweza kupata huduma zote zinazohusiana na uanachama wao popote walipo kupitia simu janja na computer, amesema Amana
Aidha, Afisa Uhusiano Mkuu wa PSSSF, Fatma Elhady, amesema, siku zote PSSSF imekuwa mstari wa mbele kushirikiana na wadau wote kuhimiza usawa kwa watu wenye ulemavu wakiwemo wenye ualbino.
“Tunashirikiana na makundi yanayojishughulisha na kuhimiza haki na usawa kwa wenye ualbino na makundi malum, kupitia sera za ndani haswa ya wajibu wa kijamii (CSR).” amesema
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED