MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), imeendelea kung’ara kwa mara ya tatu mfululizo kwa kutwaa Tuzo ya Mwajiri Bora wa Mwaka kwenye Sekta ya Umma.
TPA ilitwaa tuzo hiyo katika hafla ya usiku wa Tuzo za Waajiri Bora kwa mwaka 2024 iliyofanyika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali, ambapo mgeni rasmi alikuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, aliyemwakilisha Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango.
Mkurugenzi wa Rasilimali Watu (TPA), Mbarikiwa Masinga, alisema TPA haikuishia tu kushinda Tuzo ya Mwajiri Bora wa Mwaka kwenye Sekta ya Umma.
Alisema ilitwaa pia tuzo nyingine nne, ikiwemo Tuzo ya Mwajiri Bora Mzawa, ambayo iliiweka mamlaka hiyo kwenye nafasi ya mshindi wa kwanza.
Alisema TPA ilitambuliwa kama moja ya taasisi zinazofanya vizuri zaidi kupitia Tuzo ya “Club of Best Performers,” na pia ilipongezwa kwa uanachama wa muda mrefu wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) kupitia Tuzo ya Mwanachama wa Kudumu kwa Taasisi za Umma.
Alisema tuzo hizi hutolewa kila mwaka na ATE kwa waajiri kutoka sekta za umma na binafsi ambao wameonyesha utendaji bora na ubunifu katika mwaka husika. Ushindi wa TPA ni uthibitisho wa dhamira yake ya kuboresha ustawi wa wafanyakazi, kuboresha mazingira ya kazi, na kuendelea kuchangia maendeleo ya sekta ya bandari nchini.
Masinga alisema kwa mara nyingine TPA imeonyesha kuwa ni mwajiri wa mfano, si tu katika sekta ya umma bali pia kwa jumla katika sekta zote nchini.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED