JANGA SELIMUNDU: Serikali yaja na mambo manne ya lazima na hiari

By Sanula Athanas , Nipashe
Published at 09:31 AM Feb 03 2025
Serikali yaja na mambo manne ya lazima na hiari.
Picha: Nipashe Digital
Serikali yaja na mambo manne ya lazima na hiari.

SERIKALI imepokea mapendekezo yaliyotolewa na madaktari bingwa wa selimundu kukabili ugonjwa huo nchini, ikieleza kuwa baadhi hayatekelezeki kibajeti, pia katika uhusiano kijamii na utawala bora.

Desemba 31 mwaka jana, Nipashe ilichapisha ripoti maalum kuhusu selimundu na madhara yake kimwili, kiuchumi na kijamii, takwimu za serikali zikionesha wanazaliwa watoto 14,000 wenye maradhi hayo nchini kila mwaka huku nusu yao wakipoteza maisha ndani ya miaka mitano ya kuzaliwa kwao.

Katika ripoti hiyo ya Nipashe, madaktari bingwa wa selimundu wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam, Hospitali ya Rufani ya Kanda Bugando jijini Mwanza na Hospitali ya Rufani ya Benjamin Mkapa (BMH) jijini Dodoma walitoa mapendekezo matano kwa serikali.

Mapendekezo hayo ni pamoja na serikali kutunga sheria ya kuzuia kuoana kama hamjapimwa selimundu; wajawazito kupimwa selimundu wanapoanza kliniki; watoto kupimwa kama wana maradhi hayo mara tu wanapozaliwa; na kadi za kliniki za watoto kuwekwa alama ya kuwatambua wenye selimundu (SS) na waliobeba vinasaba vya maradhi hayo (AS).

Mabingwa hao pia walipendekeza serikali kutoa elimu kuhusu selimundu kwa jamii, ikiwezekana maradhi hayo yawe sehemu ya mtaala wa elimu kuanzia shule za msingi hadi vyuoni nchini.

Mratibu wa Huduma za Selimundu, Himofilia na Magonjwa ya Damu - Wizara ya Afya, Dk. Asteria Mpoto na Mkurugenzi Msaidizi wa Magonjwa Yasiyoambukiza - Wizara ya Afya, Dk. Omary Ubuguyu wamezungumza na mwandishi wa habari hii kuhusu hoja za mabingwa hao wa selimundu.

Wote walikubaliana na mapendekezo hayo isipokuwa hoja ya kutunga sheria inayoweka sharti la kupimwa selimundu kabla ya kuoana na kujua hali ya vinasaba vya kinamama wote wanapoanza kliniki ya ujauzito. 

SHERIA YA SELIMUNDU

Mkurugenzi Msaidizi Dk. Ubuguyu alisema pendekezo la kutunga sheria ya kuzuia wananchi kuoana kabla ya kupimwa selimundu halitekelezeki, akiwa na maelezo kuwa litaleta shida kijamii na utawala bora.

"Tukishatunga sheria hiyo, maana yake kuwe na adhabu. Tukishasema vijana wetu lazima wapimwe, waadhibiwe kwa kuoana bila kupimwa selimundu? Je, viongozi wa dini wataacha kweli kufungisha ndoa kisa wanaotaka kuoana hawajapimwa selimundu?

"Kumbuka asilimia 90 ya wanaoamua kufunga ndoa, walishaanza uhusiano zamani. Njia sahihi hapa ni kuelimisha vijana. Tuna kampeni ya 'Vunja Mduara wa Selimundu' iliyoanza mwaka jana, tunatoa elimu shuleni na vyuoni. Vijana wakishapata elimu na kupima, wanakuwa na uamuzi sahihi zaidi," Dk. Ubuguyu alisema.

Katika hilo, Mratibu wa Selimundu Dk. Asteria alisema hawajafikia hatua ya kutunga sheria kukabili selimundu na aliungana na Mkurugenzi Msaidizi Dk. Ubuguyu kwamba njia rahisi ni kutoa elimu kwa jamii kuhusu maradhi hayo.

"Hata kwenye VVU (Virusi vya Ukimwi) hatujafikia hatua ya kuwa na sheria inayozuia anayeishi na VVU kuoana na mtu mwingine anayesihi na VVU. Kikubwa kinachotakiwa ni serikali tuendelee kuelimisha jamii yetu kuhusiana na huu ugonjwa. Wakishaelewa tu basi itakuwa rahisi kuukabili," Dk. Asteria alisema. 

Nipashe Digital.

WAJAWAZITO, WATOTO

Kuhusu kuwapima selimundu wajawazito mara tu wanapoanza kliniki na baadaye watoto watakaowazaa, Dk. Ubuguyu alisema ni hoja yenye nia njema, lakini kibajeti haitekelezeki.

Mkurugenzi Msaidizi huyo alibainisha kuwa kwa wastani kila mwaka nchini kinamama milioni mbili hubeba ujauzito na kujifungua watoto milioni 2.4 (baadhi hujifungua pacha).

"Kipimo cha selimundu kinagharimu Sh. 11,000 kwa mtu mmoja. Sasa piga hesabu kwa idadi hiyo ya wajawazito na watoto wanaozaliwa, maana yake serikali itahitaji kuwa na zaidi ya Sh. bilioni 40 kwa mwaka kwa ajili ya kupima selimundu kwa wajawazito na watoto wachanga.

"Kulingana na bajeti yetu, hatutapima wajawazito na hatutapima watoto wote wanaozaliwa, bali katika kampeni yetu tutapima watoto wachanga kwenye maeneo yenye shida zaidi ya selimundu; mikoa ya Kanda ya Ziwa, Pwani na Kigoma.

"Tutaanza na mikoa ya Kanda ya Ziwa, na katika hili tuna ushirikiano na Serikali ya Marekani. Tutapima watoto 500,000 kwa mwaka. Upimaji watoto wachanga utaanza mwezi Machi mkoani Mwanza," Dk. Ubuguyu alisema.

Katika hilo, Mratibu wa Huduma za Selimundu Dk. Asteria alitaja mikoa yenye wagonjwa wengi, hata kuichagua kuanza nayo katika kampeni ya upimaji watoto wachanga, ni Mwanza, Kigoma, Geita, Shinyanga na Mara.

KADI ZA KLINIKI

Kuhusu kadi za kliniki za watoto kuwekwa alama ya kuwatambua wenye selimundu (SS), waliobeba vinasaba vya maradhi hayo (AS) na wasio na selimundu wala vinasaba vya maradhi hayo (AA), Dk. Asteria alisema hoja hiyo itafanyiwa kazi na wizara, akiwa na angalizo utekelezaji wake unagusa bajeti ya serikali.

"Zipo kadi za kliniki ambazo zilishatengenezwa na zinaendelea kutumika. Yatakapofanyika mapitio mengine ya kadi za kliniki katika miaka mitatu ijayo, watatushirikisha ili na sisi sasa tuweke vile vitu vya umuhimu ambavyo vinahitajika.

"Mpango upo wa kuhakikisha kwenye ile kadi tunaongeza huduma za sikoseli (selimundu) na ndiyo maana sasa hivi tunakwenda kupima watoto, ina maana tukishapima hawa watoto, nia yetu tuwapate kwenye kliniki," Dk. Asteria alisema.

 ELIMU SHULENI

Kuhusu utoaji elimu ya selimundu katika jamii, Dk. Asteria alisema ndicho kipaumbele cha serikali, sasa wanaelekeza nguvu kwa wanafunzi wa shule za sekondari, vyuoni na kwa wanaohudhuria kliniki za selimundu hospitalini.  

"Vilevile, tuna waraka tunatarajia kuupeleka shule za sekondari na vyuoni kwa ajili ya kupima vijana mara tu wanapoingia shuleni na vyuoni. Vijana wanapoanza tu kidato cha kwanza na chuo wafanyiwe vipimo vya selimundu. Tupo kwenye huo mchakato.

"Si unajua, mtu anapokwenda kuanza kidato cha kwanza, kuna fomu ya daktari anapima haja ndogo, macho... sasa tunataka na sisi tuweke utaratibu  apimwe vinasaba vya selimundu kwa sababu akitambua akiwa kidato cha kwanza, itamsaidia kuja kufanya uamuzi sahihi anapotaka kuoa au kuolewa.

"Wale ambao watakuwa wamebeba vinasaba vya selimundu (AS) wataendelea kupewa elimu ili watakapokuwa watu wazima, wasije wakaoa mtu mwingine aliyebeba vinasaba hivyo au mwenye selimundu tayari (SS)," Dk. Asteria alisema.

 MAWAKILI WALONGA

Wakili wa Kujitegemea, Peter Kibatala anaungana na maofisa wa Wizara ya Afya kupinga pendekezo la kutunga sheria kuzuia kufunga ndoa kabla ya kupimwa selimundu.

Katika mazungumzo na Nipashe jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Wakili Kibatala alisema: "Wanachopaswa kufanya madaktari ni kutoa ushauri kwa jamii. Wawaeleze watu madhara yanayoweza kutokea wakizaa mtoto mwenye selimundu, zikiwamo gharama kubwa za matibabu ya ugonjwa huo.

"Magonjwa si selimundu tu, kuna magonjwa mengi; ugonjwa wa moyo na kisukari ni magonjwa ya kurithi. Je, nayo tuyatungie sheria? Zitatungwa sheria kwa magonjwa mangapi?"

Wakili Kibatala aliendelea kusema: "Ukitunga sheria, lazima uweke na utekelezaji wake. Hivyo, kabla ya kutunga sheria lazima ujue sheria hiyo ina mashiko kwa uhalisia au la.

"Wameshindwa kwenye VVU/Ukimwi, wataweza kwenye selimundu? Nia ni njema, lakini hauwezi kudhibiti maambukizi kwa kutunga sheria.  Ni vyema serikali ikawekeza kwenye kufanya utafiti ili kupata ufumbuzi wa selimundu na magonjwa mengine. Tiba ya kutunga sheria ni kali sana, haitekelezeki!"

Wakati Kibatala akipinga ushauri huo wa madaktari, wakili mwenzake, Frank Chacha alisema mapendekezo ya mabingwa hao ni mazuri, akishauri muswada wa sheria ya kukabili selimundu uwasilishwe bungeni ili sheria itungwe.

"Hata kwenye CPA (Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai) na Sheria ya Ndoa kuna vifungu vinazuia ndugu kuoana, pia wenye magonjwa ya kurithi. Madaktari wako sahihi, itungwe sheria kuzuia wenye magonjwa ya kurithi kuoana, pia waliobeba vinasaba vya magonjwa hayo wasioane ili kupunguza maambukizi," alisema Wakili Chacha.

 KAULI ZA WANANCHI

Godyfrey Kweka, mkazi wa mtaa wa Nyasaka "B", kata ya Kawekamo wilayani Ilemela, akizungumza na Nipashe kuhusu mapendekezo hayo ya madaktari, alisema hoja ya kutungwa sheria ya kupima selimundu kabla ya ndoa ina mashiko na italeta mafanikio katika kukabiliana na tatizo hilo.

"Familia inapopata mtu mwenye selimundu inapitia kipindi kigumu, wakati mwingine (ugonjwa huo) huchangia ndoa kuvunjika na malezi ya mtoto huyo kubaki kwa mzazi mmoja.

"Kama unaweza kukimbia familia kisa mtoto amezaliwa na tatizo, kwa nini usipime kabla ya kuingia katika uhusiano ili kuepuka kupata mtoto wa hivyo ambaye ataishi kwa maumivu katika maisha yake yote?" Kweka alihoji.

Sundi Charles, mkazi wa Isamilo, wilayani Nyamagana, aliunga mkono pendekezo la mabingwa wa selimundu la kutunga sheria, akiamini hatua hiyo itapunguza au kumaliza tatizo la maradhi hayo nchini.

"Japokuwa italeta shida kwenye uhusiano wa watu kuvunjika, mimi ninaona ni heri uhusiano au uchumba uvunjike kuliko kuingia katika ndoa kisha mkapata watoto wenye selimundu mkazidi kuongeza tatizo ambalo linagharimu fedha nyingi katika matibabu yake. Mtoto mwenye selimundu anapitia mateso makubwa," Charles alishauri.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel, gharama za kupandikiza uloto nchini, ambayo ndiyo tiba ya selimundu, zinaanzia Sh. milioni 50 hadi 55. Kwa sasa nchini matibabu hayo yanatolewa BMH pekee. Mgonjwa asipopandikizwa uloto, fedha hizo zinatosha gharama za kliniki ya ugonjwa huo kwa miaka mitano tu kwa kila mgonjwa.

 SELIMUNDU NI NINI?

Selimundu, kama ilivyotolewa ufafanuzi na Bingwa wa Maradhi ya Watoto katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk. Evance Godfrey, ni ugonjwa wa kuzaliwa nao kutokana na kuurithi kutoka kwa wazazi kupitia vinasaba.

Ni tatizo la muda mrefu kwenye seli nyekundu za damu ambalo husababisha baadhi ya seli nyekundu za damu kuwa na umbo lisilo la kawaida. Badala ya kuwa na umbo linalofanana na diski, zinakuwa na umbo kama la nusu mwezi (mwezi mwandamo) ambalo husababisha seli nyekundu za damu kuvunjika kwa urahisi na zisitoshee vizuri katika mishipa midogo ya damu ili kusafirisha oksijeni.