Aliyekuwa Mratibu wa Habari na Mawasiliano wa timu ya kampeni ya Freeman Mbowe, Edward Kinabo, amesema kuwa Mbowe hana siasa za chuki, jambo lililoonekana wazi baada ya kukubali matokeo ya uchaguzi wa uenyekiti wa CHADEMA hadharani na kuutakia kheri uongozi mpya wa chama hicho.
Kinabo ameeleza kuwa Mbowe hakugombea uenyekiti kwa maslahi binafsi, bali kwa maslahi ya chama na taifa kwa ujumla.
“Baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi wa uenyekiti wa CHADEMA uliofanyika Januari 22, 2025, katika ukumbi wa Mlimani City, Mbowe aliwataka wanachama waendelee kushikamana na chama, wakipigania ndoto yao ya kuwakomboa Watanzania,” alisema Kinabo.
Mbowe aliwahimiza wanachama wake kutokata tamaa wala kujitenga na chama kutokana na matokeo hayo.
"Msije mkawaza kuacha siasa au kuacha chama hiki eti kwa sababu mimi mliyeniunga mkono nimeshindwa. Wala msifikirie kuususia au kuukomoa uongozi huu mpya uliochaguliwa kwa sababu tu mimi sijaibuka mshindi. Hapana, msifanye hivyo," alisema Mbowe.
Aliendelea kusisitiza kuwa ni muhimu kwa wanachama kuendelea kushikamana na chama na kupigania ndoto zao za kisiasa.
"Najua na ninyi mmekuwa na ndoto zenu za kisiasa kupitia chama hiki. Ni lazima maisha mengine yaendelee. Endeleeni kushikamana na chama, endeleeni kupigania ndoto zenu katika siasa na kuiendeleza ndoto ya chama chetu ya kuwakomboa Watanzania," aliongeza.
Kwa mujibu wa Kinabo, maneno haya ya Mbowe yanaonesha kiwango kikubwa cha busara, uungwana, na ukomavu wa kisiasa.
"Kwa uzito na mguso wa nasaha hizi, nalazimika kuziweka hadharani ili ziwe kumbukumbu na rejea kwa viongozi wa sasa na wa baadaye. Mbowe ameonesha wema na hekima ya kupigiwa mfano katika siasa za nchi yetu," alisema Kinabo.
Aidha, Kinabo alibainisha kuwa Mbowe si mtu wa kubadilika kulingana na mazingira, bali anasimamia misingi yake kwa dhati.
"Wapo viongozi wengi wanaoonesha hekima hadharani, lakini faraghani wanakuwa tofauti. Kwa Mbowe, haikuwa hivyo. Tulipoketi naye faragha nyuma ya pazia, alikuwa na msimamo ule ule. Alimaanisha alichosema hadharani na alimaanisha alichosema sirini pia," alisisitiza Kinabo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED