Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Boniface Mwambukusi, amesema kuwa TLS siyo kikundi cha kigaidi bali ni taasisi halali inayofanya kazi kwa mujibu wa sheria, ikiwa na haki ya kuishauri, kupongeza, na hata kuikosoa serikali pale inapobidi.
Akizungumza leo jijini Dodoma katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini yaliyofanyika kwenye viwanja vya Chinangali, Mwambukusi amekanusha madai kuwa uongozi wa TLS umenyamazishwa na serikali.
“Kuna watu wanaodai kuwa tumenyamazishwa au ‘tumelamba asali’, lakini ukweli ni kwamba sisi siyo kikundi cha kigaidi. Tunafanya kazi kwa mujibu wa sheria, tukiwa na uhuru wa kushirikiana na yeyote. Kama serikali imefanya vizuri, tunao wajibu wa kuisifia; na pale inapokosea, tunapaswa kuikosoa kwa maslahi ya umma,” amesema Mwambukusi.
Aidha, ameeleza kusikitishwa na baadhi ya watu wanaopinga hatua ya chama hicho kupokea gari kutoka kwa serikali kwa ajili ya kuhudumia wananchi.
"Mbona vyama vya siasa vina wabunge lakini bado vinapokea ruzuku kutoka serikalini? Leo hii kuna watu wanaopinga sisi kupewa gari, ilhali lengo letu ni kuwahudumia wananchi. Kila mtu mwenye nia njema anaweza kutusaidia ili tuendelee kutekeleza majukumu yetu kwa ufanisi," ameongeza.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED