Tulia ataka maombezi Uchaguzi Mkuu

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 11:15 AM Feb 03 2025
Spika wa Bunge, Dk.Tulia Ackson akishiriki ibada ya jumapili katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Kimara, Dar es Salaam jana.
PICHA: MPIGAPICHA WETU
Spika wa Bunge, Dk.Tulia Ackson akishiriki ibada ya jumapili katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Kimara, Dar es Salaam jana.

SPIKA wa Bunge, Dk.Tulia Ackson amewaomba watanzania kuombea Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, ili wapatikane viongozi bora na wema watakaoongoza taifa liendelee kuwa na amani.

Dk. Tulia alitoa rai hiyo jana alipokaribishwa kusalimia waumini katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Kimara mkoani Dar es Salaam wakati wa ibada ya Jumapili.

Alisema anaamini watanzania wamekuwa wakimwombea Rais Samia Suluhu Hassan na viongozi wote, lakini kwa mwaka huu ni vyema wakaelekeza maombi yao kwenye uchaguzi huo.

"Nidhahiri kwamba mnaliombea taifa hili na mnamwombea Rais Samia Suluhu Hassan, sasa wakati mwingine huwa mnamsikia akiwashukuru viongozi wa dini kwa ujumla wao kwamba wanaliombea taifa hili na anaomba waendelee kuliombea na kumwombea, lakini na ninyi wana-Kimara ni sehemu ya ambao wanamwombea mema Rais.

"Na niwaombe kipekee, tuongeze maombi zaidi kwa sababu yeye ndiye nembo ya taifa letu, ndiye Rais wetu, ndiye kiongozi wetu na pamoja na mambo mengine, mimi ni mwumini wa hapa sawa, lakini mwaka huu ni wa uchaguzi. Kwa hiyo ni vizuri watu wa Mungu tukatulia mbele za Mungu na kwa kweli kufanya yaliyo bora kabisa, siwezi kutumia madhabahu kusema mambo ya siasa na huwa sipendi kufanya hivyo.

"Lakini ni muhimu wewe umchaye Bwana, kwa sababu Biblia inasema 'maombi ya mwenye haki yafaa sana, tena ukiomba kwa bidi'. Sasa wewe mwana-Kimara maombi yako yafaa sana, tena ukiomba kwa bidi. Liombee taifa hili liendelee kuongozwa vizuri, viongozi wawe bora, ili na wewe maisha yako yastawi katika taifa hili," alisema Dk. Tulia.

Aliwataka wananchi kuacha kujiweka pembeni na kuendelea kubisha kwa kila jambo linalofanyika, akiwa na ufafanuzi: "Usijiweke tu pembeni ukafikiri wewe utakuwa tu kila wakati ubishe kila jambo linalofanyika, ubishe kila siku, kila jambo. Wewe unayemcha Mungu, kazi yako ni kupiga magoti, kwa sabahu viongozi watakaochaguliwa Biblia imekuagiza kuwaheshimu wenye mamlaka.

"Na ili umheshimu, basi mwombe Mungu atupe viongozi bora, wema, watakaolifanya taifa letu liendelee kuwa na amani, na mimi ninaamini tutaendelea kufanya vyema kwa kadri Mungu atakavyotujalia. Kwa hiyo pamoja na shukrani zote hizi kwamba mnamwombea Rais, mnaniombea mimi na viongozi wote, mnaombea amani taifa hili, lakini mwaka huu tuombee uchaguzi, Mungu atupe viongozi bora, viongozi wema."

Oktoba mwaka huu Tanzania inatarajiwa kufanya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani. Tayari Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) inafanya maboresho ya Daftari la Kudumu la Wapigakura.