Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Godfrey Nyaisa, amewataka watumishi wa taasisi hiyo kuzingatia maadili na kuweka nidhamu katika utendaji kazi, ili kuongeza ufanisi katika kutoa huduma kwa wananchi.
Nyaisa ameyasema hayo leo wakati wa kikao maalumu na watumishi wote wa BRELA, kilichofanyika mkoani Dar es Salaam kwa lengo la kukumbushana majukumu, kusikiliza changamoto za kiutendaji na kuzitatua, kuwapongeza wafanyakazi bora na kuwaaga waliostaafu.
“Napenda kuwasisitiza sana suala la nidhamu ya kazi, tujenge utamaduni wa kuheshimu nafasi tulizonazo na tuwe waadilifu mahala pa kazi, ili hata ukienda taasisi nyingine nje ya BRELA waone kweli umejifunza kazi na unaiweza,” amesema Nyaisa na kuongeza: "Kila mmoja atambue wajibu wake na kuutekeleza."
Amewakumbusha kuwa juhudi za mfanyakazi mmoja mmoja ndizo zinazompa nafasi Afisa Mtendaji Mkuu kuonekana kuwa anafanya kazi na kuipa sifa taasisi kwa ujumla.
Nyaisa amesema ataendelea kufanyia maboresho ya kiutendaji ili kutatua changamoto zilizopo.
Kikao hicho kilifuatiwa na hafla ya kuwapongeza wafanyakazi bora wa taasisi hiyo kwa mwaka 2023/2024, ambao walitunukiwa vyeti na zawadi, huku mfanyakazi Hodari wa Taasisi akipata cheti na Sh. milioni tatu.
Watumishi bora waliopata zawadi na cheti ni Vicente Nyanje, Abdulkarim Nzori, Boniface Ngugi, Abas Cothema, Gwamaka Mwankenja, Mwajabu Goma, Swedi Jabiri na Onesmo Mushi, ambaye pia amekuwa mtumishi hodari.
Katika kikao hicho pia watumishi waliostaafu waliagwa na kupongezwa kwa mchango wao walioutoa kwa taasisi, ambao wamezawadiwa vocha yenye thamani ya shilingi milioni moja kila mtumishi ambayo watakwenda kufanya manunuzi ya kitu chochote.
Wafanyakazi hao waliostaafu utumishi wao kwa mujibu wa sheria ni Deo Meela, Andrew Mkapa, Gloria Binamungu na Gloria Mbilimonywa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED