Wawili wauawa na wananchi wenye hasira kali wakishukiwa kumchoma kisu Mwanamke

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 06:28 PM Feb 03 2025
Kamanda wa Polisi  Mkoa wa Kipolisi Tarime/Rorya  SACP, Michael Njera
Picha: Mtandao
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Tarime/Rorya SACP, Michael Njera

VIJANA wawili wakazi wa Kijiji cha Remagwe Kata ya Regicheri Tarafa ya Inchugu wilayani Tarime mkoani Mara wameuawa kwa kukatwa mapanga na Wananchi wenye hasira kali wakiwatuhumu kumvamia Sofia Werema kisha kumchoma kisu sehemu mbalimbali za mwili hadi utumbo kutoka nje.

Vijana hao ni pamoja na Nyamhanga Mrimi (28) na Moris Gokoya (26) ambao wanadaiwa kukodiwa kufanya uhalifu huo huku anayesadikiwa kuwakodi akitokomea kusikojulikana.

Akielezea tukio hilo jana, Diwani wa Kata hiyo ya Regicheri Mbusiro alisema tukio hilo limetokea mwishoni mwa wiki na kuwa vijana hao walishambuliwa wakituhumia kumchoma visu Mwanamke huyo.

Alisema Mwanamke huyo aliyetambuliwa kwa jina la Sofia Werema akiwa nyumbani alivamiwa na kumchoma visu  sehemu mbalimbali  ya mwili hadi utumbo kutoka nje ambako  alikimbizwa Hoaspitali ya  Dk.Stephen  na kulazwa huko hadi sasa.

Alisema hali ya mama huyo bado haijaimarika vyema na kudai kuwa aliwatambua na kuwafahamu waliomvamia na kumchoma visu kisha kuwataja kwa ndugu zake.

"Ilikuwa Jumapili wananchi wakazi wa Kijiji hiki  walikusanyika  hapa Kijijini na kupiga Kengere na Watu wengi kujitokeza na kuanza kufanya msako kuwasaka washukiwa hao  na walipohojiwa na Wananchi hao sababu za kumshambulia Mwanamke huyo  walidai kuwa walikodishwa na Mtu mmoja  aliyetajwa kwa jina la Emanuel Yusufu,"alisema  Mbusiro.

Alidai kuwa Mtu huyo alikuwa na Kesi  ya madai Mahakama ya Mwanzo Sirari  na kuwa mama huyo aliyechomwa visu alishiriki kutoa ushahidi katika kesi hiyo hivyo lusadikiwa kukodi vijana hao wamshambulie ili kupoteza ushahidi.

Alidai baada ya Wananchi kubaini hayo walilawashambulia hadi kufa huku wakichoma mali za anayedaiwa kuwatuma vijana hao ikiwemo duka lake la dawa.

"Tunawaasa Wananchi  kutojichukulia sheria  mkononi badala yake kufikisha maswala yao kwenye vyombo  vya sheria  ili hatua zaidi ziweze kufatwa dhidi ya Watuhumiwa,"alisema  Diwani huyo.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Remagwe Wandwi Mongora  alisema tukio hilo linahusishwa na chuki na kuwa kama serikali haifurahii kuawa kwa vijana hao na kuwa wanasubiri Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wake.

Kamanda wa Polisi  Mkoa wa Kipolisi Tarime/Rorya  SACP Michael Njera alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo na kusema kuwa wanaendelea kufanya uchunguzi sababu za  mauaji hayo.

Alisema miili imehifadhiwa Chumba cha kuhifadhi maiti kituo cha afya Sirari na inatarajiwa kuchukuliwa na ndugu zao kwa ajili ya mazishi.

"Tunatoa  wito kwa Wananchi kuacha kujichukulia Sheria mikononi  badala yake  kuyafikisha malalamiko yao kwenye vyombo husika badala ya kujichukulia maamuzi kama hayo  ambayo yanaleta  chuki  na uhasama katika Jamii," alisema Kamanda Njera.