Shule yawachangia mil 14/- watoto wanaougua saratani

By Jenifer Gilla , Nipashe
Published at 10:04 AM Feb 03 2025
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Kimataifa Academic, wakifanya matembezi ya kuhamasisha kuchangia fedha kwa ajili ya kusaidia matibabu ya watoto wenye saratani, Upanga, jijini Dar es Salaam jana.
PICHA: JUMANNE JUMA
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Kimataifa Academic, wakifanya matembezi ya kuhamasisha kuchangia fedha kwa ajili ya kusaidia matibabu ya watoto wenye saratani, Upanga, jijini Dar es Salaam jana.

SHULE ya Sekondari ya Academic International imetoa msaada wa Sh. milioni 14 kwa ajili ya kusaidia matibabu ya watoto wanaougua saratani nchini.

Mkuu wa Shule hiyo, Shyama Santhosh, aliyasema hayo juzi jijini Dar es Salaam wakati wa matembezi ya kuhamasisha uchangiaji fedha kwa ajili ya kuwasaidia watoto wanaougua saratani, ikiwa ni sehemu ya Kampeni ya Piggy Bank inayoendeshwa na Taasisi ya Tumaini la Maisha.

Matembezi hayo ambayo yalianzia viwanja vya Jeshi la Ulinzi wa Wananchi (JWTZ) Upanga hadi Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), yameratibiwa na shule hiyo kwa kushirikiana na Benki ya CRDB, JWTZ na Taasisi ya Tumaini la Maisha.

Mkuu wa Shule hiyo, Shyama Santhosh, ameitaka jamii kuwa na moyo wa kujitolea kusaidia watoto wenye uhitaji kutoka kwenye makundi mbalimbali, ikiwamo wagonjwa ili kurahisisha upatikanaji wa huduma na kuwarudishia tumaini.

Alisema lengo la matembezi hayo ni kuhamasisha jamii kuchangia watoto wanaougua saratani. Mbali na kuratibu matembezi hayo, shule hiyo  ilichangia Sh. 14,080,000 kwa Taasisi ya Tumaini la Maisha kwa ajili ya mahitaji ya watoto hao, zikiwamo gharama za matibabu.

"Hii ni mara ya pili tunashiriki katika kampeni hii na safari hii tumeshirikisha wanafunzi katika matembezi, ili kuwajengea moyo wa kutoa na kuisaidia jamii, lengo ni kutengeneza kizazi chenye upendo na kujitolea, kusaidia makundi mbalimbali yenye mahitaji," alisema.

Eliwangu Mlaki kutoka Taasisi ya Tumaini la Maisha, aliishukuru shule hiyo kwa fedha walizowapa kwa kuwa zitakwenda kusaidia matibabu ya watoto wanaougua ugonjwa huo wanaopata matibabu MNH na hospitali nyingine 13 nchi nzima.

Pia aliwashukuru wadau wengine wanaowaunga mkono katika kampeni hiyo na kuratibu matembezi yanayolenga kuhamasisha jamii kutoa kuchangia fedha kwa kundi hilo.

 Meneja Uhusiano wa Benki ya CRDB, Lulu Meru, alisema wameunga mkono matembezi hayo kwa ajili ya kukusanya fedha za kuwasaidia watoto wenye saratani ili ziwasaidie katika mahitaji yao na kuwapa tabasamu.

Alisema kuwa kwa muda mrefu wamekuwa wanasaidia jamii kupitia sekta mbalimbali ikiwamo afya, hivyo wameguswa kuona kuwa katika nchi kuna watoto wanaugua ugonjwa huo.

“Sisi kama CRDB, benki ya wazalendo, tunafanya kazi karibu na jamii, tumeona tushiriki matembezi haya, ili kuhamasisha jamii kuchangia kiasi hicho cha fedha,” alisema.

Mwenyekiti wa Shule hiyo, Balozi Alli Siwa, aliwapongeza wanafunzi na wazazi walioguswa na kutoa fedha kwa ajili ya kusaidia watoto wanaougua saratani na kuwa ni matumaini yake mkakati huo utakuwa mfano wa kuigwa na jamii.

Meja Jenerali Wilbert Ibuge alisema japokuwa matembezi hayo ni mafupi, yana maana kubwa kwa kuwa lengo lake ni kutoa tabasamu na matumaini kwa watoto wanaougua saratani ambao wengine hawana uwezo wa kupata mahitaji muhimu.