Miili miwili ya wachimbaji kati ya mitatu yapatikana Kahama

By Shaban Njia , Nipashe
Published at 07:15 PM Feb 03 2025
Miili miwili ya wachimbaji kati ya mitatu yapatikana Kahama.
Picha:Shabani Njia
Miili miwili ya wachimbaji kati ya mitatu yapatikana Kahama.

Miili miwili kati ya mitatu ya wachimbaji wa madini waliokuwa wamefukiwa na kifusi katika Mgodi wa Nkadi, uliopo Mtaa wa Ilindi-Mwine, Kata ya Zongomela, Halmashauri ya Manispaa ya Kahama, mkoani Shinyanga, imeopolewa huku juhudi za kumtafuta mchimbaji mmoja zikiendelea.

Tukio hilo lilitokea Februari 1, 2025, majira ya saa nne asubuhi, baada ya kifusi kuporomoka ghafla wakati wachimbaji hao wakiendelea na shughuli za uchimbaji wa madini. Juhudi za kuwaokoa zilichelewa kutokana na uwepo wa maji mengi ndani ya duara walimokuwa wakifanya kazi.

Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Wilaya ya Kahama, ASP Stanley Luhwago, akizungumza na vyombo vya habari, amesema kuwa wamefanikiwa kuopoa miili ya wachimbaji wawili kati ya watatu waliokuwa wamefukiwa na kifusi. Hata hivyo, alibainisha kuwa zoezi la kumtafuta mchimbaji mwingine bado linaendelea kwa kushirikiana na wachimbaji wadogo.

"Changamoto kubwa ni maji mengi ndani ya duara, jambo linalotulazimu kusitisha uokoaji kwa muda ili kuvuta maji na kupata njia ya kusogea zaidi ndani ya mgodi," amesema ASP Luhwago.

Kwa upande wake, Mkaguzi Mkuu wa Migodi ya Wachimbaji Wadogo Wilaya ya Kahama, Ernest Maganga, amesema kuwa juhudi za kuopoa miili zilianza mara moja kwa kushirikiana na Jeshi la Zimamoto, na hadi sasa wamefanikiwa kuopoa miili miwili pekee.

"Wachimbaji hao walikuwa wakirekebisha pambu kwa ajili ya kuvuta maji yaliyokuwa yamejaa kwenye duara, lakini ghafla gema la udongo liliwaangukia na kuwafukia, hali iliyosababisha maafa haya," amesema Maganga.

Ameongeza kuwa baada ya zoezi la kuopoa miili yote kukamilika, watafanya ukaguzi wa kina kwenye migodi yote ili kubaini changamoto zilizopo. Migodi itakayobainika kuwa na dosari itafungwa hadi pale wamiliki wake watakapofanya marekebisho.

"Kwa sasa ni kipindi cha mvua za masika, hali inayopelekea maduara mengi kujaa maji, jambo linalohatarisha maisha ya wachimbaji. Tunawataka wamiliki wa migodi kuchukua tahadhari na kuhakikisha mazingira yao ni salama kabla ya kuendelea na uchimbaji," amesisitiza Maganga.

Kelvin Jonasi, mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, amesema kuwa siku moja kabla ya tukio, alikutana na marehemu na walikuwa naye usiku wa Januari 31, ambapo walichukua tochi na kuingia mgodini. Hata hivyo, asubuhi ya Februari 1, walipokea taarifa za kuporomoka kwa kifusi hicho.

"Mgodi waliokuwa wakitumia siyo imara, baadhi ya miundo yake imeoza na linahitaji ukarabati kabla ya wachimbaji kuendelea na shughuli zao," amesema Jonasi.

Minza Francis, ndugu wa mmoja wa wachimbaji waliopoteza maisha, alieleza huzuni yake kwa kumpoteza kaka yake, ambaye kabla ya safari yake ya Kahama alifika nyumbani kwao Mwanza na kuwaaga akisema anakwenda mashimboni kutafuta fedha.

"Alituaga kuwa anakwenda kufanya kazi ili apate fedha za kujikimu, lakini safari yake imeishia ndani ya shimo alilokuwa akitafuta riziki," amesema kwa masikitiko Francis.

Zoezi la uokoaji linaendelea, huku mamlaka zikihimiza tahadhari kubwa kuchukuliwa ili kuepusha majanga kama haya katika siku zijazo.