Majaliwa: Tutayaenzi mema ya RAS Nzunda

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:58 AM Jun 22 2024
Majaliwa: Tutayaenzi mema ya RAS Nzunda.

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema serikali na Watanzania wataendelea kumkumbuka na kuyaenzi mema yote yaliyofanywa na aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, Tixon Nzunda.

Majaliwa aliyasema hayo jana alipokwenda kuhani msiba wa Dk. Nzunda, nyumbani kwa marehemu huko Goba, wilayani Ubungo, Dar es Salaam. Dk. Nzunda alifariki dunia Juni 18 mwaka huu kwa ajali ya gari. 

"Tuna jukumu la la kumwomba Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu Nzunda pahala pema, pia tuna jukumu la kuipa faraja familia yake," Waziri Mkuu alisema.  

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - Tawa za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa alisema kuwa uwezo aliokuwa nao Dk. Nzunda ulikuwa wa aina yake na ni pigo kutokana na kazi kubwa aliyokuwa anaifanya. 

Waziri Mchengerwa alisema kuwa vijana wengi walijifunza kutoka kwake, akisisitiza, "Tuna mengi ya kusema kama ushuhuda wa yale aliyoyafanya katika kipindi chote cha uongozi wake." 

Awali mtoto wa marehemu, Victor Nzunda, alisema baba yao aliwaasa waishi maisha ya kufanya ibada, akisisitiza kuwa, "Baba yetu alikuwa mcha Mungu". 

Victor alisema baba yao alikuwa akiunganisha watu wenye mahitaji, wakiwamo yatima na wazee pamoja na kwenda hospitalini kwa ajili ya kufariji wagonjwa.