Punguzo usajili Kilimanjaro International Marathon linakaribia kumalizika

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 05:56 PM Dec 03 2024
Punguzo maalum usajili Kilimanjaro International Marathon linakaribia kumalizika.
Picha: Mpigapicha Wetu
Punguzo maalum usajili Kilimanjaro International Marathon linakaribia kumalizika.

Wakati siku za tukio la mbio za kimataifa za Kilimanjaro Premium Lager Marathon kwa mwaka wa 2025, zikikaribia washiriki wamekumbushwa kuwa muda wa punguzo la bei kwa ajili ya usajili huo unakaribia kumalizika.

Taarifa iliyotolewa na waandaaji wa hafla hiyo ambayo imekuwa maarufu Barani Afrika, imesema kuwa muda wa punguzo la hilo unatarajiwa kumalizika ifikapo Desemba 12, 2024, ambapo washiriki wamekumbushwa kuchangamkia fursa hiyo kwa kujiandikisha ili kupata namba za ushiriki, haswa ikitiliwa maanani ya kuwa siku zilizobakia kabla ya tukio hilo ni chini ya miezi mitatu kuanzia sasa.

"Kipindi cha ofa hii kilianza tarehe 21 Oktoba,mwaka huu na kitaenda hadi hadi usiku wa manane wa Desemba 12, mwaka huu; baada ya hapo ada za kujisajili zitaongezeka katika usajili wa makundi yote kwa washiriki kutoka ndani na nje ya nchi; hili ni kuanzia usiku wa manane wa kuamkia Desemba 13, mwaka huu, hadi usiku wa manane wa Februari 3, 2025 au pale tiketi zote zitakapouzwa; nafasi badi zipo na atakayekuja kwanza ndiye atakayehudumiwa kwanza”, ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Taarifa hiyo ya wandaaji inaendelea kusema kuwa washiriki wanaweza kujiandikisha kwa njia ya mtandao wa simu wa Yas (zamani Tigo) kupitia Mixx by Yas (zamani Tigopesa) kwa kupiga *150*01#, kisha bonyeza 5 LKS, kisha bonyeza 6 (Tiketi) na kufuata maelekezo ya kukamilisha usajili. Pia wanaweza kujisajili kupitia tovuti rasmi ya Kilimanjaro marathon ya www.kilimanjaromarathon.com.

“Hii inatumika katika usajili wa makundi yote ya mbio hizo ambayo ni Kilimanjaro Premium Lager KM 42 (Full Marathon), kilomita 21 Yas Half Marathon (zamani Tigo Kili half marathon) na CRDB 5Km Fun Run,” imesema taarifa hiyo ya waandaaji.

Taarifa inaendeleakusema kuwa kuwa usajili unatarajiwa kufungwa kabla ya Februari 23, 2025, ambapo tukio hilo linatarajiwa kufanyika katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU) huku likizingatia kanuni rasmi za shirikisho riadhaa la kimatifa (IAAF) zinazohusiana na maswala mengine, usalama wakati wote wa tukio hilo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, usajili wa mapema utatoa fursa kwa wandaaji kwashiriki wanashiriki vyema bila kuwa na changamoto yoyote ikiwemo ile msingamano wakati wote wa mbio hizo, sambamba na mipango mingine kama ile ya kuweka maji kwenye vituo mbalimbali kwa ajili ya washiriki na mipango ya huduma za kwanza pale zitakapohitajika.

Kilimanjaro Premium Lager ndio wadhamini wakuu wa mbio za marathon na imeshikilia nafasi hiyo tangu kuanzishwa kwa mbio hizo miaka 23 iliyopita.

Wadhamini wengine wa hafla ya mwakani ni pamoja na Yas (km 21) na Benki ya CRDB ya 5Km Fun Run. Wafadhili wasaidizi - Simba Cement, Kilimanjaro Water, TotalEnergies, na TPC Sugar Ltd. Wasambazaji rasmi -GardaWorld Security, CMC Automobiles, Sal Salinero Hotel na wauzaji - Kibo Palace Hotel na Keys Hotel. Mbio za mwaka ujao zitakuwa Jumapili Februari 23, 2025 katika Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU), ambapo njia zitakazotumiwa na washiriki zimepimwa na kuidhinishwa na IAAF.

Mbio za Kilimanjaro Premium Lager International Marathon zitazotarajiwa kufanyika Jumapili Februari 23, 2025, zimeandaliwa na Kilimanjaro Marathon Company Limited na kuratibiwa hapa nchini na ya Executive Solutions Limited. Taasisi ya Wild Frontiers ndiyo inayowajibika kwa usafiri wote wa ndani na maswala yote ya masoko yanayohusiana na tukio la Kilimanjaro Premium Lager International Marathon.