Bahati Nasibu ya Taifa ya Tanzania inayo furaha kutangaza ushirikiano wa kimkakati na Shirika la Posta Tanzania, wenye lengo la kuongeza upatikanaji wa michezo ya kubahatisha kote nchini. Kupitia ushirikiano huu, majukwaa ya Bahati Nasibu ya Taifa yatapatikana katika ofisi 207 za Posta, hatua itakayorahisisha upatikanaji wa michezo ya kubahatisha kwa Watanzania wanaoishi mijini na vijijini.
Kupitia mtandao mpana wa Shirika la Posta, wenye jumla ya ofisi 430 zinazotoa huduma kwa watu 79140 kwenye kila kituo, Mtandao huu utatoa jukwaa madhubuti kwa Bahati Nasibu ya Taifa kufanikisha azma yake ya kuwafikia Watanzania wote. Kwa kuunganisha majukwa ya bahati nasibu katika vituo hivi, Bahati Nasibu ya Taifa itahakikisha hata wale wanaoishi maeno yasiofikika kwa urahisi wanapata fursa ya kushiriki katika michezo hii.
Akizungumza wakati wa utiaji saini baina ya pande hizi mbili, Kelvin Koka, Mkurugenzi wa Ithuba Tanzania,amesema:
"Ushirikiano na shirika la posta Tanzania ni hatua kubwa sana ya dhamira yetu ya kuhakikisha kuwa kila mtanzania anaweza kushiriki katika michezo ya kubahatisha. Kwa kutumia mtandao mpana na wakuaminika wa shirika la posta, tutafanikiwa kuwafikia watu wote nchi zima, na kuhakikisha kila mmoja anapata nafasi ya kushiriki katika michezo ya kubahatisha. Hivyo basi ushirikiano huu ni uthibitisho wa dhamira ya ujumuishi kwa maendeleo ya taifa.
Naye Constantine John Kasese, ambaye ni Mkurugenzi wa Biashara za Kielektroniki na Huduma za Kifedha wa Shirika la Posta Tanzania, ameongeza kuwa:
"Sisi kama Shirika la Posta Tanzania, tumejikita katika kuwaunganisha watu na huduma muhimu kote nchini. Ushirikiano baina yetu na Bahati Nasibu ya Taifa unawiana na maono yetu ya kutoa huduma zinazoendana na mahitaji ya wateja wetu. Kupitia upatikanaji wa majukwaa ya bahati nasibu katika ofisi zetu,Itasaidia kuleta urahisi wa upatikanaji wa tiketi za michezo ya kubahatisha na kuchangia juhudi za taifa za kuwainua wananchi wetu.
Kwa kutumia miundombinu madhubuti ya Shirika la Posta Tanzania, Jukwaa la Bahati Nasibu ya Taifa linalenga kutoa michezo iliyo rafiki, rahisi, na yenye uwazi kwa washiriki wote, ikiimarisha dhamira yake ya kuboresha maisha ya Watanzania kote nchini.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED