Siri ya Chelsea kurundika wachezaji wengi vijana

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 05:35 PM Mar 24 2025
Geovany Quenda alisajiliwa na Chelsea kutoka Sporting wiki hii kwa pauni milioni 42
Picha: Mtandao
Geovany Quenda alisajiliwa na Chelsea kutoka Sporting wiki hii kwa pauni milioni 42

WINGA wa Sporting, Geovany Quenda, 17, atajiunga na Chelsea mwaka 2026, wakati kiungo Dario Essugo, 20, atahamia msimu huu kuchukua nafasi ya Moises Caicedo.

Ripoti ya hivi karibuni ya Uefa ilitangaza kikosi cha Chelsea cha 2024, kuwa kikosi cha bei ghali zaidi kuwahi kusajiliwa. Ni asilimia 24 kikosi ghali kuliko rekodi ya Real Madrid ya 2020.

Ripoti hiyo pia inasema Chelsea imetumia karibu euro bilioni 2 (£1.7bn) kununua wachezaji katika kipindi cha miaka mitano hadi 2024. Na bado wanaendelea kununua.

Vijana wengine kadhaa wanasubiri kujiunga na Chelsea katika madirisha yajayo ya uhamisho, kwa ada ya zaidi ya pauni milioni 150 kwa jumla.

Mbinu yake ni kununua nyota wachanga kwa bei ya chini, kuwalipa mishahara polepole ndani ya mikataba yao ya muda mrefu, kubadilisha wachezaji na kuuza wachezaji wasiohitajika kwa faida, na kujaribu kusaka ushindi wakati huo huo.

Wakiwa na wastani wa umri wa miaka 23 na miezi mitano, The Blues tayari wana kikosi kichanga zaidi kwenye Ligi ya England - na wanatarajiwa kuwa na kikosi kichanga zaidi kuanzia msimu ujao.

Klabu hiyo imekuwa na mabadiliko makubwa katika mkakati wa kununua wachezaji tangu Todd Boehly na Clearlake Capital kuchukua mikoba ya Roman Abramovich mwaka 2022.

Wachezaji wengi wa zamani wa Abramovich wameuzwa katika jaribio la kupunguza wachezaji wa umri mkubwa katika kikosi - na bili kubwa za mishahara.

Pesa hizo zimewekezwa kwa vipaji vya vijana wadogo katika kile kinachoonekana kuwa mbinu ya kubadilisha biashara katika ununuaji wa wachezaji.

Wachezaji wachanga wanasainiwa kwa mikataba mirefu, kwa kawaida kati ya miaka saba na tisa. Mmiliki mwenza Boehly wa timu hiyo alieleza sababu ya kufanya hivyo katika hafla ya mwezi uliopita ya FT Business of Football.

"Unatafuta wachezaji wachanga, ili wawepo na wategemewe kwa muda mrefu - na hilo ni chaguo la thamani. Siku zote unawekeza kwenye kukiweka kitu pamoja kwa muda mrefu."

Ripoti ya hivi karibuni ya CIES Football Observatory, ilifichua kuwa Chelsea ndio timu inayofanya vizuri zaidi katika soka duniani – kwa kupima dakika ngapi (karibu 92%), zinachezwa na wachezaji walio na mikataba inayovuka mwaka 2026.

Ni mtindo unaoweza kuleta utulivu" katika miaka ijayo kwa timu au "kuleta faida kubwa" kutokana na uhamisho.

Chelsea inatafuta vijana wengi wenye viwango vya juu kutoka kote ulimwenguni kwa matumaini watazalisha nyota wakubwa kama Cole Palmer au Nicolas Jackson.

Pia wanataka kuvishinda vilabu kama Benfica kwa kuzalisha vipaji katika soko la soka kama vile Amerika Kusini, ili kuepuka kulipa malipo makubwa kama walivyofanya wakati wa kumsajili Enzo Fernandez kwa pauni milioni 107 mwaka 2023.

Winga wa Ukraine, Mykhailo Mudryk - ambaye alijiunga na Chelsea kwa pauni milioni 89, kutoka Shakhtar Donetsk mwaka 2023 - analipwa pauni 97,000 tu kwa wiki kwenye mkataba unaoendelea hadi 2031. Ni mfano mmoja wa jinsi wachezaji wanavyoweza kupata mishahara midogo huku wakiwa na mikataba mirefu.

Mudryk kwa sasa amesimamishwa kucheza baada ya kugunduliwa kuwa na dawa iliyopigwa marufuku. Iwapo atapatikana na hatia, anaweza kupigwa marufuku ya miaka minne, huku akiwa bado na mkataba wa kulipwa wa miaka kadhaa na Chelsea.

Na vipi ikiwa mchezaji anataka kuondoka? Kwenye podikasti ya Overlap, Jamie Carragher aliuliza kama klabu yoyote inaweza kumudu kumnunua nyota wa Chelsea aitwaye Palmer.

Mwaka jana, mchezaji huyo aliongeza mkataba wake hadi 2033. Na itakuwaje kama ataudhika na atataka kuondoka kutokana na wachezaji wenzake kutocheza chini ya viwango.

Ili kumnunua mchezaji, timu inayotaka kumnunua inapaswa kulipa kiasi chote cha pesa ya mshahara wa mchezaji ndani ya kipindi kilicho baki cha mkataba wake. Hapa ndipo swali linapoibuka, ikiwa mikataba hiyo ya miaka minane, ni nzuri kwa klabu na wachezaji.

Pia kuna wachezaji wachanga kama Cesare Casadei, Renato Veiga na Carney Chukwuemeka ambao wote waliondoka Chelsea mwezi Januari huku kukiwa na wasiwasi wa kukosa nafasi ya kucheza, kwani nyota wengi wachanga wanawania nafasi hizo.

Kuna swali pia, ikiwa Chelsea hailipi mishahara ya kiwango cha juu: Je, wachezaji bora watajiunga na klabu hiyo? Na uzoefu wa mchezaji una maana yoyote kwa Chelsea?

Wamiliki wa Chelsea, na wale walio karibu nao, daima wameeleza hamu yao ya kushinda na kufikia matarajio yao ya muda mrefu.

Hata hivyo, wanataka kuyafanikisha hayo kwa mbinu hii ya sasa na wametaka washabiki kuwa na uvumilivu, kusubiri wachezaji wao na mradi huu kufikia hatua ya kukomaa.

Chanzo kimoja kimeiambia BBC Sport kwamba mradi huo uko katika 'Everest Base Camp' - mahali pa kuanzia kupanda mlima huo mkubwa zaidi duniani.

Chelsea inaamini kocha Enzo Maresca anafanya kazi vizuri ndani ya mradi huo kuliko watangulizi wake Mauricio Pochettino na Thomas Tuchel, huku akipata matokeo bora kuliko Graham Potter - ambaye alifukuzwa kutokana na matokeo mabovu.

BBC