BUNGE limeipa jukumu Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kufanya utafiti wa kina kuhusu mkanganyiko wa sheria unaotoa adhabu ya viboko kwa kijana mwenye miaka 18 aliyetiwa hatiani kwa kosa la ubakaji kwa madai kuwa ni mtoto.
Spika wa Bunge, Dk.Tulia Ackson, aliyasema hayo juzi bungeni baada ya kuipa nafasi serikali kutafuta majibu sahihi kufuatia maswali ya nyongeza ya Mbunge wa Viti Maalumu (CHADEMA), Agnesta Kaiza.
Katika maswali yake, Mbunge huyo alisema Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, inamtambua kijana wa miaka 18 kama mtu mzima, lakini katika sheria ya kupambana na masuala ya ubakaji, kijana wa miaka 18 anatambulika kama mtoto mdogo.
“Kijana huyu akienda kubaka, adhabu yake ni kupigwa viboko. Je, serikali haioni sheria hii imepitwa na wakati na hivyo kusababisha mgongano na Katiba mama?
“Na mko tayari kupitia upya sheria hii ili kuendana na wakati na kujulikana wazi kama kijana wa umri huo ni mtoto atakuwa hana sifa hizi zingine kama kupigakura, kuchaguliwa kuwa kiongozi na zinginezo?”alihoji
Hata hivyo, kutokana na swali hilo, Spika Tulia aliomba wabunge wabobezi wa sheria na serikali kujiridhisha kama kuna sheria inayotoa adhabu hiyo ili kutoa majibu sahihi kwa umma.
Kabla ya kumaliza kipindi cha maswali na majibu, Spika Dk. Tulia alitoa fursa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari, kutoa ufafanuzi na alikiri uwapo wa adhabu hiyo.
Alisema Sheria ya Kanuni za Adhabu kifungu cha 131(2) imeweka angalizo kuwa kama makosa hayo yametendwa na mvulana ambaye ana umri chini ya miaka 18 na kama ni mara yake ya kwanza atapata adhabu ya viboko.
Johari alisema adhabu hiyo inakinzana na Sheria ya Mtoto kupitia kifungu cha nne ambacho kimetafsiri vizuri kwamba, mtoto ni yule ambaye yupo chini ya miaka 18.
Hata hivyo, alisema ofisi yake inalichukua suala hilo kwenda kuliangalia na kulifanyia utafiti ili kuona kama kuna haja ya sheria hiyo kuandikwa upya.
“Tutafanya utafiti kwanini tulikuja na suala hili la mtoto wa miaka 18 asifungwe kifungo cha maisha, ili tuweze kufanya maamuzi sahihi,” alisema.
Kutokana na ufafanuzi huo, Spika Tulia, alisema Bunge limeiachia kazi ofisi hiyo kwenda kufanya utafiti kuhusu sheria hiyo.
“Tumewaachia mwende kufanyia kazi suala hili labda wakati wanatunga walikuwa na sababu na kama zimebadilika na kama kuna sababu ya hapa na pale basi tufanye marekebisho.
“Nakumbuka iliwahi kuletwa hoja kutoka Iringa, ililetwa na Mbunge Rose Tweve, kifungu hiki kilileta mgogoro yaani, mtu alikuwa ana miezi miwili ndio ametimiza miaka 18 halafu akabaka mtoto ikawa shughuli, inabidi aadhibiwe kama mtu mzima au kifungu hiki anakua nacho,”alisema.
Alisema kutokana na mkanganyiko wamewaacha wafanye utafiti ili kuwa na ulinzi wa watoto na kila mmoja alindwe na sheria hiyo.
Awali, katika swali la msingi, Mbunge Agnesta alihoji kiwango gani sheria zilizopo za kupambana na matukio ya ubakaji zinajitosheleza.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Geofrey Pinda, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, alisema Mwaka 1998, Bunge lilitunga aheria mahususi inayosimamia makosa ya kujamiiana na makosa yanayoendana nayo.
Alisema sheria hiyo ilifanya marekebisho ya Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16; Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Sura ya 20; Sheria ya Ushahidi, Sura ya 6; Sheria ya Ukomo wa Adhabu, Sura ya 90; na iliyokuwa Sheria ya Mtoto na Mtu mwenye Umri Mdogo, Sura ya 13.
“Lengo la kutungwa kwa sheria hiyo ilikuwa ni kumlinda mwanamke na mtoto dhidi ya makosa ya kujamiiana na makosa yote yanayoshabihiana. “Sheria hii iliongeza adhabu ya makosa hayo kuwa ni kifungo cha maisha au kifungo kisichopungua miaka 30 jela,” alisema.
Alisema kwa kiasi kikubwa sheria zilizopo zinajitosheleza kupambana na matukio ya ubakaji.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED