CHAMA cha Wananchi (CUF) kinatarajiwa kuzindua rasmi kampeni zake leo jijini Mwanza kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, huku kikitangaza vipaumbele 10 vitakavyotekelezwa endapo kitaingia madarakani.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mgombea Urais wa CUF, Gombo Samandito , amesema serikali yake inalenga kujenga taifa lenye usawa, heshima na furaha kwa wananchi wote.
Gombo ametaja maeneo 10 ya kipaumbele ambayo chama chake kitaweka mkazo iwapo kitapata ridhaa ya kuongoza nchi ikiwemo huduma za afya bure ili wananchi wote wapate matibabu bure bila bima ya afya, kwa kuwa huduma za afya ni haki ya msingi kwa kila Mtanzania,elimu bila malipo kuanzia elimu ya awali hadi chuo kikuu itatolewa bure, huduma za umeme na maji zitatolewa bure kwa wananchi wote.
Pia ajira kwa vijana serikali ya CUF itatoa ajira kwa vijana waliohitimu vyuo mbalimbali, na kujaza nafasi za watumishi serikalini, wakulima, wafugaji na wavuvi watawezeshwa ili kuongeza uzalishaji na kipato kila mtumishi mpya atapewa hati ya kiwanja na nyumba ya kuishi, pamoja na kuhakikisha kikokotoo cha pensheni kinafutwa ,serikali itaruhusu uraia pacha ili kuimarisha mchango wa Watanzania wanaoishi nje ya nchi.
Anaeleza kuwa serikali yake itapunguza kodi nyingi na kubaki na kodi moja tu kwa mwaka, Serikali itaanzisha utaratibu wa makazi kwa kujenga nyumba katika miji mikuu ikiwemo Dar es Salaam, Dodoma, Arusha, Mbeya na Mwanza na Serikali itawekeza kwenye teknolojia ya kidijitali, kutoa leseni za uchimbaji kwa uwazi, na kufuta TFS (Tanzania Forest Services) ili kuondoa migogoro baina ya wafugaji na mamlaka hiyo.
Gombo alisisitiza kuwa dira ya CUF inalenga kuondoa tofauti za kipato na kuhakikisha kila Mtanzania anashiriki kikamilifu kwenye "keki ya taifa." “Kila mtu lazima awe na furaha. Serikali ya CUF itajenga taifa lenye usawa, ambapo kila mmoja ataona matunda ya uhuru wake,” alisema.
Hata hivyo amesema endapo CUF itashika madaraka suala la kupotea watu halitakuwepo kwani litahakikisha vyombo vya dola vinafanya kazi yake kwa ufasaha kwa kuendelea kulinda wananchi na kuishi katika usalama.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Habari wa CUF, Rajabu Mbaramwezi, msafara wa kampeni utaanza leo saa 3:00 asubuhi katika eneo la Rwagasole (Nyamagana), kisha kupita maeneo ya Igogo Senta, Mkuyuni, Nyegezi, Mkolani, Buhongwa, Rwanhima, Igoma, Nyakato Sokoni, Nyakato Meco, Mlango Mmoja, Nata na Milongo Sokoni. Baadaye, msafara utaingia Uwanja wa Furahisha ambapo mkutano mkubwa wa hadhara utafanyika kuanzia saa 8:00 mchana.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED