Katibu Mkuu wa zamani CCM, Dk. Bashiru Ally, amesema nguvu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na uwezo wake unatokana na umoja ndani ya chama na umoja wa kitaifa.
Amesema Mwenyekiti wa Chama hicho, Rais Samia Suluhu Hassan, ameisimamia kazi ya kuunganisha chama na kuunganisha taifa. Ametoa kauli hiyo leo Agosti 31, 2025, wilayani Kondoa, mkoani Dodoma, katika mkutano wa kampeni ya mgombea urais wa chama hicho.
“Ujumbe wangu kwa Watanzania na wana CCM nguvu ya Chama Cha Mapinduzi na uwezo wake ni umoja wa chama na umoja wa kitaifa. Ninakushuku Mheshimiwa Mwenyekiti kwa kuchukua kazi hiyo ukiwa kiongozi na kuisimamia kazi ya kuunganisha chama na kuunganisha taifa,” amesema.
Dk. Bashiru amewaeleza wananchi kuwa nchi inaendelea vizuri maeneo mengi, hivyo wako katika kunadi wagombea wao na kuendelea kushirikana na CCM.
Katika mkutano huo, Dk. Bashiru amesema amepewa kazi na Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya chama hicho, kuratibu shughuli za kampeni na tayari Mwenyekiti wao ameshawapa maelekezo ya nini cha kufanya kuomba kura nyumba kwa nyumba, kitongoji kwa kitongoji na mtaa kwa mtaa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED