Mgombea Urais wa Chama cha National League for Democracy( NLD) Doyo Hassan Doyo amesema endapo watanzania watampa ridhaa ya kuongoza nchi, atapambana na rushwa kwenye miradi ya maendeleo na kuweka sheria kali ikiwemo wahusika kunyongwa.
Doyo ametoa kauli hiyo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye Ofisi za Chama hicho zilizopo Tandika jijini Dar es Salaam, kuhusu uzinduzi wa kampeni za Chama hicho zinazotarajiwa kufanyika Septemba 4,2025 jijini Tanga.
“Rushwa imekuwa chanzo cha miradi kukwama kwa sababu ya kugawana asilimia. Serikali ya NLD haitavumilia wala kufumbia macho tatizo hili,” amesema Doyo.
Ameahidi kuimarisha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU na mamlaka nyingine zinazohusika na udhibiti ili kuhakikisha rasilimali za taifa zinawanufaisha Watanzania wote.Amewataka watanzania kujitokeza kwa wingi kumuunga mkono wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu, akiahidi mageuzi makubwa ya kiuchumi.
Ameongeza kuwa NLD imesimamisha wagombea 100 wa nafasi ya Ubunge ambao tayari wamekabidhiwa fomu ya kugombea nafasi zao, vilevile wagombea 1000 wa nafasi ya Udiwani.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED