KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti imesema hadi Juni 2024, deni la serikali lilikuwa Sh. trilioni 96.88 ikilinganishwa na Sh. trilioni 81.98 katika kipindi kama hicho mwaka 2023, sawa na ongezeko la asilimia 18.18.
Aidha, imeishauri serikali mambo manne ya kuhakikisha deni la serikali linaendelea kuwa himilivu.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Oran Njeza, aliyasema hayo bungeni juzi alipokuwa akisoma maoni ya kamati kuhusu mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2025/26 pamoja na mapendekeo ya mwongozo wa maandalizi ya Mpango na Bajeti ya serikali kwa Mwaka 2025/26.
Alisema ongezeko hilo la asilimia 18.18 ni sawa na Sh. trilioni 14.90 na kati ya deni hilo la ndani lilikuwa Sh. trilioni 31.95 na nje lilikuwa Sh. trilioni 64.93.
“Uchambuzi wa Kamati umebaini kwamba, mpaka sasa deni la serikali ni himilivu kwa kipindi kifupi, cha kati na kirefu. Ongezeko la deni limesababishwa na kushuka kwa thamani ya shilingi pamoja na kupokea mikopo mipya kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo,” alisema.
Hata hivyo, alisema kamati hiyo inashauri serikali kuongeza wigo na ukusanyaji wa mapato ya ndani ili yawe na uwezo wa kugharamia deni, mikopo yote inayopatikana ni vema serikali ikaielekeza katika miradi inayochochea kasi ya ukuaji wa uchumi na mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi.
Alisema lengo ni kuhakikisha hawafiki katika ukomo wa ulipaji wa deni la nje kwa uuzaji wa bidhaa nje ambao hivi sasa tupo asilimia 11.1 na ukomo ni asilimia 15.
“Kutoa kipaumbele kwa mikopo yenye masharti nafuu na yenye masharti ya kati ili kupunguza mzigo wa riba pamoja na muda mfupi wa neema ambao unaambatana na mikopo ya kibiashara na kutafuta vyanzo vingine bunifu vya mapato kama vile hatifungani za kijani, diaspora, manispaa na miundombinu,” alisema.
Akizungumzia hali ya umaskini na maendeleo ya watu, Njeza alisema kamati inaishauri serikali kutenga bajeti kwa mwaka wa fedha 2025/26, kwa ajili ya kufanya utafiti wa mapato na matumizi ya kaya ili kupata takwimu ya hali ya umaskini nchini kwa kuwa taarifa ya mwaka 2017/18 imepitwa na wakati.
“Kamati inaishauri serikali kuhakikisha kwamba, ongezeko la watu linaendana na ukuaji wa uchumi kwa sababu, hivi sasa kati ya watu 100 watu 87 ni tegemezi,” alisema.
SGR NA MGR
Alisema kamati inashauri kutenganisha usimamizi wa reli ya Kisasa ya SGR na reli ya MGR na kulifanya Shirika la Reli nchini (TRC) kuwa Shirika Hodhi linalosimamia Mashirika mawili.
“Serikali itumie mpango wa kufadhili ujenzi wa Reli ya Kisasa ya SGR kwa kutumia ECGA (Export Credit Guarantee Agency) ili kukamilisha vipande vyote vilivyobaki kwa haraka hususan vipande vya Uvinza - Malagarasi- Msongati na Kaliua- Mpanda- Karema,” alisema.
Alisema kamati inaishauri serikali, kuongeza safari za ndege katika maeneo ambayo wana uhusiano mkubwa wa kibiashara, sambamba na kuboresha viwanja vya ndege vya ndani kwa kuviwekea taa, ili kuongeza idadi ya miruko ya ndege za ATCL ndani ya nchi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED