KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti imesema watu 87 kati ya 100 ni tegemezi nchini, hivyo kushauri itengwe bajeti ya kufanya utafiti wa mapato na matumizi ya kaya, ili kupata takwimu ya hali ya umaskini.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Oran Njeza, aliyasema hayo bungeni juzi alipokuwa akisoma maoni ya kamati kuhusu mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2025/26 pamoja na mapendekeo ya mwongozo wa maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2025/26.
Alisema kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, idadi ya watu ilikuwa 61,741,120 mwaka 2022 na inakadiriwa kuwa ifikapo mwaka 2035 idadi ya watu nchini itakuwa 87,509,630 kutokana na ongezeko la asilimia 3.2 kila mwaka.
“Ongezeko hili la idadi ya watu nchini haliendani na ukuaji wa uchumi. Kamati inaishauri serikali kuhakikisha kwamba, ongezeko la watu linaendana na ukuaji wa uchumi kwa sababu hivi sasa, kati ya watu 100 watu 87 ni tegemezi,”alisema.
Aidha, alisema kamati inaishauri serikali kutenga bajeti kwa mwaka wa fedha 2025/26, kwa ajili ya kufanya utafiti wa mapato na matumizi ya kaya ili kupata takwimu ya hali ya umaskini nchini kwa kuangalia viashiria vyote 17 kutokana na taarifa iliyoko hivi sasa ya hali ya umaskini ni ya mwaka 2017/18 na imepitwa na wakati.
Alisema Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025 ilibainisha kwamba ili Tanzania iondokane na umaskini ni lazima uchumi ukue kwa asilimia nane hadi 10.
“Kamati inashauri kuwa sekta ya kilimo ina uhusiano mkubwa na hali ya umaskini nchini ambapo jumla ya watu milioni 28 sawa na asilimia 45.9 ya watu wote Tanzania wanajishughulisha na sekta ya kilimo.
“Kamati inaishauri serikali kuhakikisha kwamba, inakamilisha miradi yote ya kilimo kwa wakati ili kupunguza hali ya umaskini nchini. Mfano, mradi wa Kujenga Kesho iliyo Bora (BBT) na ujenzi wa mabwawa ya umwagiliaji,” alisema.
DARAJA LA BUSISI
Alisema kamati inaishauri serikali kuhakikisha daraja la Kigongo - Busisi linakuwa la kulipia ili kupata fedha zitakazotumika katika kufanya ukarabati wa daraja hilo.
Alisema kamati inaishauri serikali kuhakikisha kwamba, miundombinu ya usambazaji wa umeme inaimarishwa ili kuimarisha upatikanaji wa umeme kwa wananchi.
“Hivi sasa taifa lina ziada ya umeme wa Megawati 606.04. Hata hivyo, ziada hiyo inaweza kuwa inatokana na wananchi wengi kutounganishwa kwenye gridi ya taifa na kutowafikia wananchi kutokana na ubovu wa miundombinu,” alisema.
Njeza alisema kamati imefanya uchambuzi na kubaini kuwa sekta ya ujenzi wa barabara inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo utekelezaji kutokuzingatia ujenzi wa barabara za kimkakati, kuanza ujenzi wa barabara nyingi kwa pamoja bila kuzingatia uwezo wa kifedha.
Pia, alisema malimbikizo ya madeni ya wakandarasi na kusababisha sehemu kubwa ya bajeti kutumika kulipa madeni ya miaka ya nyuma.
Alishauri serikali kutoa kipaumbele katika ujenzi na ukarabati wa barabara za kimkakati na zenye manufaa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED