SHIRIKA la Nyumba Zanzibar (ZHC) limedaiwa kukosea kuwataka wakazi wa nyumba za Mjeruamani zilizoko Kikwajuni, kuhama kabla ya nyumba hizo kuvunjwa kupisha uwekezaji, likidaiwa majengo hayo si mali ya ZHC.
Mvutano huo umewaibua watu kadhaa akiwamo mtoto wa pili wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Balozi Ali Abeid Karume, ambaye ndiye aliyebariki ujenzi wa makazi hayo.
Aidha, umemwibua pia aliyekuwa Mbunge wa Kikwajuni, Parmukh Hoogan Sigh.
Balozi Karume alisema kitendo kitakachofanya wananchi wanaoishi katika nyumba hizo kuhamishwa kinaweza kuzua mtafaruku.
“Majengo ya mjerumani si miliki ya Shirika la Nyumba Zanzibar bali yako chini ya dhamana ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ). Yamejengwa na Ujerumani ili wananchi wanyonge waishi. Madai yoyote ya kuwaondoa wakazi wake yanaweza kutaleta hekaheka kubwa,” alisema.
Singh alisema kuvunjwa nyumba hizo kutafuta historia kati ya Ujerumani na Zanzibar kwa sababu ndiyo waliojenga baada ya Mapinduzi.
Ujerumani Mashariki ndiyo taifa la kwanza kuyatambua mapinduzi ya Zanzibar mwaka 1964, ikafuatia China kabla ya mataifa mengine duniani kufanya hivyo.
“Majengo yale yana siasa kwa upande mmoja, pia historia na utalii. Kuyavunja na kubadilisha matumizi ni kuvuruga uhusiano na ushirikiano. Ni vema ikashauri Ujerumani ili ivunje na kujenga mengine kuliko kufuta alama yao kihistoria,” alisema Singh.
Aliongeza kuwa itakuwa busara Ujerumani ikashirikishwa mapema, kwani hata kiongozi wake alitembelea Zanzibar.
Mwenyekiti wa kamati ya kufuatilia mgogoro huo, Jaha Ame Rajab, alisema tayari wananchi wameanza vikao vya kujadili suala hilo na viongozi wa SMZ.
Jaha alisema Mkuu wa Wilaya ya Mjini ameshakutana na kamati yake, hivyo kuna vikao vinavyoendelea ambavyo bado haijajulikana hatima yake.
“Kuna familia nyingi zinaishi katika majengo ya Mjerumani. Kuziondoa familia hizo iki kupisha uwekezaji si jambo la kufumba na kufumbua macho wala kuchukuliwa kwa pupa,” alisema Jaha.
Alikumbusha kuwa watu wanaishi tangu awamu ya kwanza, hivyo uamuzi wowote wa kuwafukuza, unaweza kuleta manung'uniko yasiokwisha na kushangaza.
Aidha, Chama cha ACT Wazalendo kilisema uamuzi huo unakwenda kinyume na malengo ya Abedi Amani Karume ya kuwapatia wananchi makazi bora.
Waziri Kivuli wa Ardhi, Maji, Nishati wa ACT Wazalendo, Rashid Ali Abdalllah, alisema kinachoendelea katika majengo hayo si jambo jema.
“Yawapo mazungumzo kati ya wakazi na SMZ. Ikiwa ni fidia walipwe na kama kutakiwa kuhama hadi ujenzi utakapokamilika wapewe fedha za kujikimu kimaisha si kuwaondoa kinyume na utu wa mtu” alisema Abdallah.
Ghorofa za Kikwajuni zilijengwa baada ya mapinduzi kama msaada wa kuwapatia makazi bora wananchi kazi iliyofanywa na Serikali ya Ujerumani Mashariki.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED