JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, limesema linamtafuta Mkurugenzi wa Dar24, Maclean Mwaijonga, anayedaiwa kupotea kwa takriban siku nne hadi sasa.
Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Jumanne Muliro, alisema jana kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari kwamba familia yake imeripoti tukio la kupotea kwa Mwaijonga katika Kituo cha Polisi Oysterbay.
Alisema imeripotiwa kwamba Mwaijonga ambaye pia alikuwa mfanyakazi katika Kampuni ya Data Vision International Ltd, iliyoko Mikocheni, Dar es Salaam, hakurudi nyumbani kwake tangu alipoingia kazini Oktoba 31, mwaka huu.
Alisema pia, gari yake namba T 645 DEE, aina ya Toyota Prado, aliyokuwa anaitumia siku hiyo, nayo haionekani.
“Uchunguzi na ufuatiliaji wa taarifa hiyo unafanywa na polisi kwa kushirikiana na ndugu, ili kujua na kubaini mtu huyo yupo wapi.
“Jeshi la Polisi linatoa wito kwa yeyote mwenye taarifa kuhusiana na mtu huyo azitoe katika mamlaka yoyote ya serikali iliyo karibu yake,” alisema Kamanda Muliro katika taarifa hiyo.
Awali, kampuni ya Dar24 Media iliripoti kupotea kwa Mwaijonga ambaye hajulikani aliko tangu alipoonekana Oktoba 31, mwaka huu, saa 11:00 jioni alipokuwa akitoka ofisini kwake, DataVision International Ltd, Mikocheni.
Mkurugenzi wa Biashara wa DataVision International, MacMillan George, alisema: “Dar24 Media inaomba atakayemwona au kuwa na taarifa za Mwaijonga au gari lake, atoe taarifa kupitia namba O713249003.”
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED