Serikali yataja hatua nane kuboresha uwekezaji

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:03 PM Jan 10 2025
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo
Picha:Mtandao
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo

SERIKALI imeainisha hatua nane za kuboresha uwekezaji nchini ikiwamo kutoa vibali kwa Watanzania wanaoishi nje ya nchi kufungua vituo vya uhamasishaji uwekezaji na kuanza kutekeleza ujenzi wa miundombinu katika maeneo maalum ya kiuchumi ikiwamo Bagamoyo.

Aidha, kwa mwaka 2025, serikali imejiwekea lengo la kuvutia miradi mipya 1,500 ya uwekezaji na mitaji ya Dola za Kimarekani bilioni 15 ifikapo Desemba, mwaka huu.

Sekta mahsusi ni viwanda, kilimo, uchukuzi, nishati safi, utalii, madini na huduma, ongezeko litakaloifanya Tanzania kuwa moja ya nchi tano bora katika uwekezaji barani Afrika kwa wingi wa mitaji.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, jana alikuwa akitoa mwenendo na hali ya uwekezaji nchini katika kipindi cha miaka mitatu ya awamu ya sita ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, alipokuwa akizungumza na wahariri na wamiliki wa vyombo vya habari nchini.

Hatua zingine zilizoainishwa ni kutunga Muswada wa Sheria Mpya ya Uwekezaji Tanzania ambao pamoja na mambo mengine, unapendekeza kuunganisha taasisi za TIC na EPZA. Muswada huo uliwasilishwa Bungeni mwaka 2024 na sasa uko katika ngazi ya Kamati ya Kudumu ya Bunge kwa ajili ya kufanyiwa kazi.

Aidha, kuandaa awamu ya pili ya Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji (MKUMBI). Ni baada ya kufanya tathmini ya utekelezaji wa MKUMBI I uliobaini mafanikio mbalimbali katika kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji.

Pia, tathmini hiyo ilibaini changamoto mpya zilizojitokeza ambazo serikali na wadau wanaendelea kuzifanyia kazi. Lengo ni kuifanya Tanzania kuwa moja ya nchi zenye mazingira bora ya kufanya biashara na uwekezaji barani Afrika.

Hatua zingine alizozitaja ni kuanzisha utaratibu wa kuzipima mamlaka za serikali za mitaa katika kuboresha mazingira ya biashara na kuhamasisha na kuwezesha uwekezaji. Kuanza kutekeleza ujenzi wa miundombinu katika maeneo maalum ya kiuchumi ikiwamo Bagamoyo (Bagamoyo Special Economic Zone) ili kuwezesha ujenzi wa viwanda.

Prof. Mkumbo pia alisema serikali itaendelea kuhamasisha uwekezaji wa ndani ukiwa na lengo la kufikisha asilimia 50 ya miradi yote ya uwekezaji kwa mwaka imilikiwe na Watanzania.

“Tutashirikiana na taasisi mbalimbali za serikali kuwalenga wawekezaji wa ndani hasa wawekezaji wadogo wanaokua.  Kuboresha na kuwezesha ofisi za sekretarieti za mikoa katika kuhudumia na kuboresha mazingira ya uwekezaji katika ngazi na mikoa na wilaya nchini kote. 

“Kwa mwaka 2025, tutaanza na kufungua ofisi ya Kanda ya TIC mkoani Njombe ili kusogeza huduma za uwekezaji mkoani Njombe, Iringa na Ruvuma,” alisema.

MIRADI ILIYOSAJILIWA 2024

Prof. Mkumbo alisema hadi Desemba, 2024, TIC ilikuwa na miradi 13,282 ya uwekezaji iliyosajiliwa na kutekelezwa nchini, ikivutia mitaji kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 127,176 na kutoa ajira zaidi ya milioni 1.98.

Alisema mafanikio katika sekta ya uwekezaji yamechochewa na sababu mbalimbali ikiwamo kuendelea kuimarisha mifumo ya kisera na sheria katika kuwezesha na kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini, maono, hamasa na ushawishi ambao umeendelea kufanywa na Rais Samia kwa kampuni mbalimbali za kimataifa kuja kuwekeza nchini kupitia ziara na mikutano mbalimbali aliyoifanya nje na ndani ya nchi.

Pia kampeni kubwa ya kitaifa ya uhamasishaji uwekezaji nchini iliyofanyika mwaka jana kwa ushirikiano mkubwa katika ya TIC, chemba za biashara nchini (TCCIA, TWCC), benki, na vyombo vya habari. Jumla ya wafanyabiashara 1,800 walifikiwa kupitia kampeni hiyo katika mikoa 26 ya Tanzania Bara.

Kadhalika, katika kipindi cha Januari hadi Desemba, mwaka jana, TIC ilisajili  miradi 901 ikilinganishwa na 526 iliyosajiliwa katika kipindi kama hicho mwaka 2023. 

WAWEKEZAJI 7 WATIA FORA

Aliwataja wawekezaji saba wanaofanya vizuri kuwa ni pamoja na Hoteli ya Southern Sun, iliyowekeza Dola za Kimarekani milioni 2.7, Kunduchi Mall, iliyowekeza Dola milioni 20, ujenzi majengo ya makazi na biashara, Dola milioni nne, Kiwanda cha Tumbaku, Dola milioni sita na DP World, iliyowekeza Dola milioni 200.

MIKOA 5 KUVUTIA WAWEKEZAJI

Prof. Mkumbo aliitaja mikoa hiyo na wawekezaji kwenye mabano kuwa ni Dar es Salaam (356), Pwani (166), Arusha (64), Dodoma (47) na Mwanza (36).

Aidha, kuanzia Januari hadi Desemba 2024, miradi 901 ilisajiliwa na kuzalisha ajira zaidi ya 200,000.