Vijana kujadili fursa za masoko, uzalishaji kilimo

By Gwamaka Alipipi , Nipashe
Published at 04:47 PM Jul 04 2024
Mkurugenzi Mkazi wa AGRA, Vianey Rweyendela ( kulia) akiwa na Mratibu wa Programu ya BBT kutoka Wizara ya Kilimo, Vumilia Zikankuba.
Picha: Gwamaka Alipipi
Mkurugenzi Mkazi wa AGRA, Vianey Rweyendela ( kulia) akiwa na Mratibu wa Programu ya BBT kutoka Wizara ya Kilimo, Vumilia Zikankuba.

VIJANA zaidi ya 100 wanatarajia kukutana na kujadiliana namna ya kujenga mazingira wezeshi ya ujasiriamali, fursa za masoko, pamoja na na uzalishaji katika kilimo.

Mkurugenzi Mkazi wa Taasisi ya Mapinduzi ya Kijani Afrika (AGRA), Vianey Rweyendela, aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam kuelekea Mkutano wa Sera wa Vijana na Ubadilishaji wa Mifumo ya Chakula, utakaofanyika Julai 5, jijini Dar es Salaam.

Alisema mkutano huo utawakutanisha vijana, washirika wa utekelezaji, wadau muhimu katika mlolongo wa thamani ya mifumo ya chakula ili kujua mahitaji na vipaumbele ya vijana katika kilimo.

Alisema mkutano huo utafanikisha hatua za sera muhimu za kuwawezesha vijana katika kilimo, kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na kuhakikisha mabadiliko katika mifumo ya chakula.

"Lengo la mkutano huo ni kuunga mkono ushiriki wa vijana katika mifumo ya chakula inayostahimili mabadiliko ya hali ya hewa na hati ya kumbukumbu ya michango ya vijana katika kuimarisha na kukuza programu zinazolenga vijana." alisema Rweyendela.

Alisema mada zitakazojadiliwa ni pamoja na upatikanaji wa ardhi, fedha, huduma za maendeleo ya biashara, utetezi wa sera, na kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Hivyo, aliwahimiza vijana kushiriki, kuchukua fomu katika jukwaa la kidijitali la AGRA.

Mratibu wa Programu ya BBT, kutoka Wizara ya Kilimo, Vumilia Zikankuba, alisema wizara ina lengo la kutoa mwongozo wa sera na huduma kwa mfumo wa kilimo na ushirika ulioimarishwa kibiashara, wenye ushindani na wenye ufanisi.

Alisema: "Serikali inajitahidi kutoa huduma za kilimo na ushirika zenye ubora, kutoa mazingira mazuri kwa wadau, kuimarisha uwezo wa mamlaka za serikali za mitaa na kuwezesha sekta binafsi kuchangia kwa ufanisi katika uzalishaji endelevu wa kilimo, tija na maendeleo ya ushirika”.