WMA waendelea kutoa elimu ya vipimo sabasaba

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 04:27 PM Jul 04 2024
WMA waendelea kutoa elimu ya vipimo sabasaba
Picha: Maulid Mmbaga
WMA waendelea kutoa elimu ya vipimo sabasaba

WAKALA wa Vipimo Tanzania (WMA) wameendelea kutoa elimu ya vipimo kwa watanzania, wakiwasisitiza kuhakikisha kila mita wanayoitumia ikiwemo ya maji na umeme iwe imefanyiwa uhakiki kabla ya kuiingiza katika matumizi.

Akizingumza leo mkoani Dar es Salaam, katika maonyesho ya 48 ya biashara ya kimataifa (Sabasaba) Meneja wa WMA Mkoa wa Iringa, Lina Msuya, amesema kutumia mita zilizofanyiwa vipimo ni muhimu kwakuwa itawasaidia kufanya malipo sahihi ya fedha yanayoendana na matumizi yao.
 
Amesema ni muhimu mwananchi yoyote kuhakikish anatumia mita yenye nembo ya WMA ili kuepuka kuingia gharama zisizoendana na matumizi yake.
 
“Mita za maji na umeme ambazo ni mpya kabla mteja hajafungiwa mamlaka husika wanazileta kwetu kwaajili ya kufanyiwa uhakiki, na ambayo itakutwa iko vizuri inawekwa nembo ya WMA inayoonyesha kwama kifaa hicho kiko tayari kwa matumizi,” amesema Lina.
 
Ameongeza kuwa jitihada hizo zinafanyika kwa dhima ya kuhakikisha kwamba wanamlinda mlaji ili awe analipa bili ya maji au umeme inayoendana na matumizi yake halisiå.
 
Aidha, ameeleza kuwa pia wanatoa elimu kuhusiana na vifaa vinavyotumika kwaajili ya kupima mita ambazo tayari ziko katika matumizi ili kumfanya mwananchi awe na uelewa kwa uwanda mpana juu uya suala hilo.
 
Pia amesema kwa mwananchi ambaye tayari ameshafungiwa mita lakini akahisi kwamba bili anayoletewa ni kubwa kuliko matumizi yake aandike barua kwa wakala wa vipimo au apige simu bure kwa namba 0800 110097.
 
“Lakini kwa yule ambaye hafungiwa bado basi ahakikishe mita atakayofungiwa iwe imehakikiwa na wakala wa vipimo kwa maana kwamba lazima iwe na nembo ya WMA, na ile ambayo haijahakikiwa na tayari iko kwenye matumizi itafanyiwa uhakiki kwa gharama za mamlaka zinazohusika,” amesema Lina.