Mabaki ya ndege iliyombeba Makamu wa Rais wa Malawi,Saulos Chilima yamepatikana bila mtu yeyote aliyenusurika, Rais Lazarus Chakwera amesema.
Chilima na watu wengine tisa walikuwa wakisafiri nchini humo jana Jumatatu asubuhi wakati ndege yao ilipotoweka kwenye rada za uwanja wa ndege.
Ndege hiyo kijeshi, ilikuwa ikisafiri hali mbaya ya hewa.
Wanajeshi walikuwa wakipekua Msitu wa Chikangawa katika juhudi za kuitafuta ndege hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 11, 2024, Rais Chakwera amesema Kamanda wa Jeshi la Ulinzi la Malawi alimweleza kuwa shughuli ya utafutaji na uokoaji imekamilika na ndege hiyo kupatikana huku watu wote waliokuwemo kufariki dunia.
Chakwera amesema "alihuzunishwa na kusikitika sana" kuwafahamisha Wamalawi kuhusu mkasa huo mbaya.
Amesema timu ya uokoaji ilikuta ndege hiyo ikiwa imeharibika kabisa.
Makamu wa rais na rais wanatoka vyama tofauti lakini wawili hao waliungana kuunda muungano wakati wa uchaguzi wa 2020.
Dk Chilima (51) alikuwa akielekea kuiwakilisha serikali katika mazishi ya aliyekuwa waziri wa serikali Ralph Kasambara aliyefariki siku nne zilizopita.
Mke wa Rais wa zamani Shanil Dzimbiri pia alikuwa kwenye ndege hiyo, iliyopaa kutoka mji mkuu, Lilongwe, Jumatatu asubuhi.
Dk Chilima amekuwa Makamu wa Rais wa Malawi tangu 2014.
Alipendwa sana nchini Malawi, hasa miongoni mwa vijana, shirika la habari la AFP linaripoti.
Hata hivyo, Dk Chilima alikamatwa na kufunguliwa mashtaka mwaka 2022 kwa madai kwamba alikubali pesa ili kutoa kandarasi za serikali.
Mwezi uliopita, mahakama ilitupilia mbali mashtaka hayo, bila kutoa sababu za uamuzi huo.
Dk Chilima ameoa na ana watoto wawili
Saulos Chilima ni nani?
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED