MKURUGENZI Mtendaji wa Benki ya Dunia (WB) Kanda ya Afrika, Dk. Zarau Kibwe, amepongeza serikali nchini na namna inavyosimamia kwa ufanisi miradi ya maendeleo, akieleza kuwa hadhi ya Tanzania kimataifa imeimarika, na sasa inatambulika kama moja ya mataifa yanayoendeshwa kwa ufanisi barani Afrika.
Pia ameupongeza uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, akieleza kuwa ni chanzo cha kuongezeka kwa kiwango cha mkopo ambacho Tanzania inaweza kupata kutoka benki hiyo kutoka Dola za Marekani bilioni tano (zaidi ya Sh. Trilioni 10) hadi Dola bilioni 12 (zaidi ya Sh. Trilioni 25).
Dk. Kibwe ameyasema hayo leo akiwa jijini Washington, Marekani wakati akizungumza na Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, aliyemtembelea ofisini kwake, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kukutana na wadau wa sekta ya ujenzi na kuhudhuria mikutano ya kimataifa.
"Sijui huko nyumbani kama mnaliona au kulizungumza hili. Katika muda mfupi ambao Rais Samia ameingia madarakani, ukomo wa Tanzania kwenye uhusiano wake na Benki ya Dunia umeongezeka kutoka dola bilioni tano hadi bilioni 12. Hili si jambo la kawaida," amesema Kibwe.
Naye, Waziri Ulega amempongeza Kibwe kwa kushika wadhifa huo mkubwa kama Mtanzania, akisema kuwa Watanzania wanajivunia mafanikio yake. Pia, ametumia fursa hiyo kueleza maendeleo ya miradi inayofadhiliwa na Benki ya Dunia, ikiwemo ujenzi wa barabara, mwendokasi na madaraja.
“Nimepata sifa zako nyingi sana kabla ya kuonana nawe. Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba alinipa sifa zako lakini pia kule nyumbani kwa sababu taasisi hii inagusa maisha ya wengi, habari zako zinajulikana sana. Hongera sana na kazi iendelee,” amesema Ulega.
Kadhalika, Waziri Ulega amegusia changamoto ya wakandarasi wa kigeni kuchelewesha miradi, akipendekeza kwamba wanapaswa kufungua akaunti Tanzania ili kuwezesha malipo kufanyika haraka na miradi isikwame.
“Kuna tatizo la hawa wakandarasi kutokuwa na akaunti nyumbani. Sasa ninyi ndiyo mnaowalipa. Sisi tunaona ni vyema hizi kampuni ziambiwe zilipe haraka ili kazi ziendelee au wafungue akaunti zao Tanzania ili iwe rahisi kwao kulipa na mambo yasilale,” amesema.
Katika majibu yake, Kibwe amemhakikishia Waziri Ulega kuwa Benki ya Dunia itaendelea kushirikiana na Tanzania, huku akimpongeza kwa msukumo mkubwa katika sekta ya ujenzi.
"Niliona mabadiliko makubwa Dar es Salaam na nikaambiwa ‘there is a new sheriff in town’. Hongera sana kwa kazi nzuri, mambo yako yanaonekana," amesema Kibwe.
Benki ya Dunia pia imethibitisha kuunga mkono mradi mkubwa wa barabara kuelekea Kusini mwa Tanzania, ikiwemo ujenzi wa Daraja la Mzinga eneo la Kongowe, Dar es Salaam.
Kibwe ni Mtanzania wa pili kushika wadhifa huo wa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia Kanda ya Afrika inayohusisha takribani nchi 23. Mtanzania wa kwanza alikuwa Christopher Kahangi aliyeshika wadhifa huo kati ya mwaka 1968 hadi mwaka 1970.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED