Majaliwa: Bil 1.5 kuimarisha mtandao wa barabara Nzega

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 04:53 PM Mar 13 2025
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa mwaka 2025/26, imetenga takribani Sh. Bilioni 1.5 kwaajili ya uimarishaji wa mtandao wa barabara za ndani kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Nzega mkoani Tabora.

Ameyasema hayo leo akiwa ziarani mkoani Tabora, ambako ameeleza kuwa yote hayo ni muendelezo wa utekelezaji wa dhamira ya kiongozi huyo wa taifa katika kuiunganisha mikoa yote nchini kwa barabara za lami na kukarabati barabara za ndani ili ziweze kutumika nyakati zote.

"Kazi hiyo inaenda sambamba na uimarishaji wa huduma ya usafirishaji katika maeneo mengine ikiwemo ununuzi wa ndege na upanuzi wa viwanja vya ndege pamoja na ujenzi wa reli na ununuzi wa mabehewa na treni kwaajili ya kusafirisha abiria na bidhaa mbalimbali," amesema Majaliwa.