TAKWIMU za Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), zinaonesha kuwa asilimia saba ya watu nchini Tanzania, wanaugua ugonjwa sugu wa figo.
Hata hivyo, idadi ya wagonjwa wanaohitaji huduma ya uchujaji wa damu (dialysis), inaongezeka kutoka 380 mwaka 2014/2016 hadi 2,900 mwaka 2021/2022 na sasa ni 3,500.
Bingwa wa Magonjwa ya Figo kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk. Jonathan Mngumi, ameeleza hayo leo, akitoa elimu kuhusu ugonjwa ya figo na magonjwa yasiyoambukiza.
Elimu hiyo imetolewa kwa walimu wakuu wa shule za sekondari jijini Dar es Salaam pamoja na polisi kutoka Chuo cha Taaluma ya Polisi (DPA), ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa afya ya kiungo hicho, kuadhimisha Siku ya Figo Duniani.
Amesema kuwa ugonjwa wa figo unawaathiri zaidi watu wenye umri wa miaka 40-50, ambao ni sehemu muhimu ya nguvu kazi ya jamii na hii inaonesha changamoto kubwa katika kupambana na ugonjwa huu, hasa kutokana na ongezeko la mahitaji ya huduma za afya.
Aidha, bingwa huyo amesema wagonjwa wanaofanyiwa huduma ya ‘dialysis’ hivi sasa imefikia 3,500.
Awali, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Dk. Faraja Chiwanga, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Huduma za Tiba, amesema kuwa lengo kuu la kuadhimisha siku hiyo, ni kuendelea kuelimisha jamii kuhusu afya ya figo, ikiwa ni pamoja na njia bora za kujikinga na magonjwa sugu ya figo ambayo yanatajwa kuwa tishio kwa jamii.
"Tunatumaini kuwa walimu hawa wataweza kufikisha elimu hii kwa wanafunzi wao, hivyo kuwajengea msingi wa afya bora ya figo tangu wakiwa vijana.
“Watakuwa mabalozi na wahamasishaji wakubwa wa afya ya figo katika familia zao, jamii zao na hata maeneo yao ya kazi," amesema Dk. Faraja.
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Ralph Meela na Mwenyekiti wa Wakuu wa Shule za Sekondari Dk. Mavumba Hussein wameushukuru uongozi wa MNH kuwapa elimu hiyo na kusema watakua mabalozi wazuri sehemu zao za kazi na jamii inayowazunguka.
Kauli mbinu ya mwaka huu ni ‘JE FIGO YAKO IKO SALAMA? Tutambue mapema, ilinde afya ya figo yako’.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED