Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (MISA) – Tawi la Tanzania, imeipongeza bodi iliyomaliza muda wake kwa mchango wao katika kukuza taasisi hiyo na kuwatuza kwa heshima. Pia, bodi mpya imesisitizwa kuendeleza umoja na kulinda mali za taasisi.
Waliopewa tuzo ni aliyekuwa Mwenyekiti wa MISA, Salome Kitomari, Makamu Mwenyekiti James Malengo, pamoja na wajumbe Mussa Juma, Michael Gwimila, na Idda Mushi.
Tuzo hizo zilikabidhiwa leo jijini Dodoma na Mkurugenzi Msaidizi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Renatus Mkude, katika mkutano wa MISA na wadau mbalimbali. Mkude ameipongeza bodi iliyomaliza muda wake kwa kazi nzuri na kusisitiza kuwa mafanikio yanahitaji bidii na kufuata utaratibu.
"Unapotaka mabadiliko lazima ufanye jambo jipya. Tuzo hizi ziwe chachu ya mshikamano na kusaidia bodi mpya kuifikisha MISA pale inapostahili," amesema Mkude.
Aidha, amewataka waandishi wa habari kufanya kazi kwa bidii licha ya changamoto zilizopo katika sekta hiyo.
Kwa upande wake, Salome Kitomari amewashukuru wanachama kwa ushirikiano waliompatia wakati wa uongozi wake na kuhimiza mshikamano na bodi mpya.
"Tumelinda mali za taasisi hadi tumekabidhi kwa bodi mpya. Ikiwa kuna lawama, basi ziwe kwa mambo mengine, siyo wizi au upotevu wa mali za taasisi," amesema Kitomari.
Pia amewataka viongozi katika vyama mbalimbali kufanya kazi kwa uwiano bila ubaguzi, akisisitiza kuwa yeye alifanikiwa kudhibiti changamoto hizo, jambo lililoisaidia MISA Tanzania kufikia hatua iliyo nayo leo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED