Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Masha Mshomba, amesema Mfuko unaendelea kutimiza azma ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kupanua wigo wa hifadhi ya jamii ili kuwafikia wananchi waliojiajiri.
Mshomba ameyasema hayo Machi 14, 2025, jijini Dar es Salaam, wakati wa uzinduzi wa Bodi mpya ya Wadhamini ya NSSF, hafla iliyoongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete.
Ameeleza kuwa kujiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii ni ajenda muhimu duniani na kwa Tanzania, ambapo Serikali ya Awamu ya Sita imetoa kipaumbele maalum kwa suala hilo. Kupitia kampeni ya "NSSF Staa wa Mchezo", Mfuko unalenga kuhakikisha wananchi waliojiajiri wanajiunga na kunufaika na mafao mbalimbali.
“Kupitia hifadhi ya jamii, mwanachama anakuwa na uhakika wa maisha na kipato hata baada ya kustaafu. NSSF ni ‘Staa wa Mchezo’ kwa sababu inahakikisha unakuwa na maisha bora sasa na baada ya kustaafu,” amesema Mshomba.
Kwa upande wake, Waziri Ridhiwani amesisitiza kuwa kampeni ya "NSSF Staa wa Mchezo" inalenga kuwahamasisha wananchi kutoka sekta mbalimbali kama kilimo, uvuvi, ufugaji, madini, bodaboda, mama/baba lishe, na wajasiriamali kujiunga na Mfuko ili kufaidika na mafao ya muda mrefu na mfupi.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mary Maganga, amewataka wajumbe wa Bodi mpya kusimamia Mfuko kwa uadilifu, huku Mwenyekiti wa Bodi, Mwamini Malemi, akiahidi kufanya kazi kwa kufuata sheria na miongozo kwa manufaa ya wanachama wa NSSF.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED