MRATIBU wa malipo ya kielektroniki kutoka Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) Josephine Joseph, amesema wamepiga hatua katika suala la uhawilishaji na kusaidia kaya maskini nchini kwa kufikia kusomesha watoto hadi vyuo vikuu na tayari mtoto mmoja ameshamaliza stashahada yake mwaka jana.
Mratibu huyo amesema hayo leo kwenye mkutano wa wanachama wa Chama cha Waandishi wa Habari wa Kusini mwa Afrika (MISA-TAN) na wadau wa habari nchini ambapo anasema watoto wa kaya maskini wamekuwa wakienda shule na kufaulu kwenye mitihani yao ya darasa la saba na sekondari na wengine kutakiwa kwenda shule na vyuo vikuu.
Amesema, walifanikiwa kuongea na bodi ya mikopo na kukubaliana kuwapa asilimia 100 ya mikopo watoto wanaotoka kwenye kaya maskini na kufanya mtoto huyo kumaliza elimu yake.
Anasema mpaka sasa TASAF imefikisha makundi 68,000 nchi nzima ambayo yamefanikiwa kuweka akiba ya Shilingi Bilioni 7.8 baada ya kupata fedha za uhawilishaji kwa ajili ya miradi.
Hata hivyo anasema kwa mujibu wa utafiti uliofanywa mwaka 2018 na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa kaya umebaini kuwa isingekuwepo TASAF kiwango cha umaskini nchini kingeongezeka kutoka asilimia 7 hadi 8.
Hivyo amevipongeza vyombo vya habari nchini kusaidia kuelimisha jamii kuhusiana na masuala ya TASAF ambayo mwanzoni yalichukuliwa kama sio njia sahihi ya kusaidia jamii kwa lengo la kukuza maendeleo kiuchumi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED