Kamati ya miundombinu yajivunia bandari ya Tanga

By Hamida Kamchalla , Nipashe
Published at 03:21 PM Mar 14 2025
KAMATI ya kudumu ya bunge ya miundombinu
PICHA: MTANDAO
KAMATI ya kudumu ya bunge ya miundombinu

KAMATI ya kudumu ya bunge ya miundombinu imetembelea kukagua miradi mitatu ya uboreshwaji wa uwanja wa ndege, reli pamoja na bandari ambapo pia watatembele ujenzi wa barabara ya Tanga - Pangani, katika Mkoa wa Tanga.

Akiongea kabla ya kuanza ukaguzi wa miradi hiyo Mwenyekiti wa kamati hiyo Suleiman Kakoso amesema lengo la ziara hiyo ni kukagua kabla ya kikao cha bajeti cha bunge ili kama  kuna changamoto itakayojitokeza katika miradi hiyo, kuweza kuijengea hoja.

Kakoso amesema kamati hiyo inajivunia kasi kubwa ya maendeleo kwenye bandari ya Tanga iliyoboreshwa na serikali ya awamu ya sita ambapo imeshuhudia mabadiliko makubwa ikilinganishwa na miaka mitatu iliyopita.

"Kamati hii ilifanya ziara bandarini hapa na kubaini kuwepo kwa uhitaji wa maboresho ili uweze kuchangia ufanisi katika mpango wa kuifanya Tanga kuwa Mkoa wa kimkakati kiuchumi na kibiashara" amesema.

Amebainisha kwamba katika kipindi hicho, kamati pia ilibaini ucheleweshwaji wa malipo kwa maboresho katika bandari hiyo, hivyo iliwapasa kuishauri serikali kutoa fedha zilizoainishwa na bunge kwa ajili hiyo.

"Nilitembelea bandarini hapa na kamati hii mwaka 2023 tukaikuta katika hali isiyoridhisha na miundombinu duni isiyokidhi ufanisi na ushindani wa soko, lakini fedha nyingi zilizotolewa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan  zimefanya maboresho makubwa na kuleta maendeleo makubwa sana" amesema