Prof. Janabi rasmi mchuano kiti Mkurugenzi WHO Kanda Afrika

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 11:38 PM Mar 14 2025
Prof. Janabi rasmi mchuano kiti Mkurugenzi WHO Kanda Afrika
Picha: Nipashedigital
Prof. Janabi rasmi mchuano kiti Mkurugenzi WHO Kanda Afrika

PROFESA Mohamed Janabi, jina lake limetangazwa rasmi kuwa miongoni mwa wagombea watano katika kuwania nafasi ya Mkurugenzi wa Kanda ajaye wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa Kanda ya Afrika.

Prof. Janabi, ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) anawania kiti hicho pamoja na wenzake miongoni mwao kutoka nchi za Afrika Magharibi.

Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika, limetoa taarifa hiyo. Majina ya wagombea hao ambayo yatafanyiwa mchakato wa Uchaguzi Mei 18, mwaka huu, yaliwasilishwa na Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk. Tedros Adhanom Ghebreyesus.

Nchi wanachama yaliwasilishwa majina hayo kwa kiongozi huyo, Leo, Machi 14, 2025 huku nchi tano ikiwamo Tanzania na nyingine nne Ivory Coast; Togo; Niger na Guinea pia wakifanya hivyo.
Wagombea kutoka nchi zingine ni Dk. N'da Konan Michel Yao kutoka Ivory Coast;  Dk. Dramé Mohammed Lamine (Guinea); Dk. Boureima Hama Sambo (Niger) na Pr Mijiyawa Moustafa wa Togo.

Hatua hiyo imekuja, kufuatia kifo cha ghafla Cha Mkurugenzi Mteule wa Kanda hiyo, Dk. Faustine Ndugulile, Novemba 2024.

Kamati ya Kanda ya WHO kwa Afrika, ilifanya kikao maalum kwa njia ya mtandao Januari 14, 2025, ili kuamua utaratibu wa uchaguzi wa Mkurugenzi wa Kanda ajaye.

Kamati iliamua kutumia utaratibu wa haraka, ili kupendekeza na kuteua Mkurugenzi wa Kanda ajaye. 

Nchi wanachama zilialikwa kuwasilisha mapendekezo kwa nafasi ya Mkurugenzi wa Kanda kabla ya Februari 28, 2025. 

Baada ya hapo, jukwaa la wateule wa wagombea litaandaliwa kwa njia ya mtandao Aprili 2, 2025.

Nchi yoyote ya Kanda inaweza kupendekeza mgombea kwa nafasi ya Mkurugenzi wa Kanda. 

Mkurugenzi wa Kanda anachaguliwa kwa kura ya siri katika kikao cha faragha cha Kamati ya Kanda.

Kikao maalum cha ana kwa ana cha Kamati ya Kanda ya Afrika, kitaandaliwa Mei 18, 2025 huko Geneva, Uswisi, ili kuteua Mkurugenzi wa Kanda ajaye.

Mkurugenzi wa Kanda anateuliwa na Bodi ya Utendaji ya WHO, baada ya uteuzi wake na Kamati ya Kanda ya WHO kwa Afrika. 

Uteuzi wa Mkurugenzi wa Kanda hiyo, utakuwa wa miaka mitano na atakuwa na haki ya kuteuliwa tena mara moja pekee.