Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Nickson Simon, ameipongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kwa utoaji wa huduma bora kwa wananchi wa wilaya yake pamoja na kuchochea uwekezaji kupitia upatikanaji wa maji ya uhakika.
Akizungumza leo, Machi 14, 2025, wakati wa kufungua Kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa DAWASA katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere mkoani Pwani, Mheshimiwa Nickson alisema kuwa uhalali wa Serikali unategemea utoaji wa huduma za msingi kwa wananchi, hivyo DAWASA inawajibika kuhakikisha huduma za majisafi na majitaka zinapatikana kwa ufanisi.
"Maji yanaweza kuleta amani au machafuko, hivyo ni muhimu kuhakikisha wananchi wanapounganishiwa huduma ya maji, yanapatikana bila changamoto," amesema.
Ameongeza kuwa DAWASA imechangia heshima ya Mkoa wa Pwani kwa kuwezesha uwekezaji, kwani uwepo wa maji ya kutosha unahamasisha maendeleo ya sekta ya viwanda.
"Wawekezaji wanapokuja Pwani tunawahakikishia upatikanaji wa maji wa kutosha, jambo ambalo limeongeza uwekezaji katika mkoa wetu," amesisitiza.
Mkuu huyo wa wilaya aliihimiza DAWASA kuongeza kasi ya utoaji wa huduma kwa wananchi, kuhakikisha upotevu wa maji unadhibitiwa, na kuendelea kuboresha huduma.
Kwa upande wake, Kaimu Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Mkama Bwire, alieleza kuwa asilimia kubwa ya vyanzo vya maji vinavyotumiwa na Dar es Salaam na Pwani vipo mkoani Pwani, akitaja mitambo ya Ruvu Juu, Ruvu Chini, na Wami kama vyanzo vikuu vya uzalishaji maji.
Aidha, ameshukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufanikisha utekelezaji wa miradi ya maji yenye thamani ya Shilingi trilioni 1.19 katika kipindi cha miaka minne.
"Kati ya miradi hiyo, Shilingi bilioni 796.19 ni kwa miradi ya majisafi, huku bilioni 400.91 zikitumika katika miradi ya usafi wa mazingira," amesema.
Mhandisi Bwire amebainisha kuwa miradi ya maji iliyokamilika ina thamani ya Shilingi bilioni 344.67, huku miradi ya majisafi ikiwa na thamani ya bilioni 329.97 na miradi ya usafi wa mazingira ikiwa na bilioni 14.7. Miradi inayoendelea ina thamani ya bilioni 852.43, ikiwa na miradi ya majisafi yenye thamani ya bilioni 466.22 na usafi wa mazingira bilioni 386.21.
Amesema idadi ya wateja wa maji safi imeongezeka kutoka 343,019 hadi 455,720, sawa na ongezeko la wateja 112,701.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED